Bahman 22 ya Mapinduzi ya Kiislamu; "Kujitawala, Kuwa Huru, Jamhuri ya Kiislamu"
(last modified Sun, 11 Feb 2018 15:42:25 GMT )
Feb 11, 2018 15:42 UTC

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameingia katika mwaka wake wa 40 wa umri wake wenye baraka tangu yalipopata ushindi siku kama ya leo miaka 39 iliyopita. Ni mapinduzi ambayo, kwa kusimama kwake kidete na imara kukabiliana na ubeberu wa madola makubwa, yameonyesha kuwa yanataka Iran iwe na uhuru wa kweli wa kujitawala; kujitawala ambako kumepatikana kwa kutegemea irada ya wananchi walioungana na kuwa kitu kimoja.

Miaka 39 ya umri wa kujivunia wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu imejaa harakati, kujitawala na izza ya taifa ambalo, kwa umoja na mshikamano wake limeweza kuzishinda njama za maadui zake.

"Kujitawala" na "Uhuru" ni miongoni mwa kaulimbiu kuu za matakwa ya wananchi Waislamu wa Iran katika kipindi cha mapambano yao ya kupigania kuwa na Jamhuri ya Kiislamu. "Kujitawala", ambalo ni moja ya matakwa makuu katika kipindi hicho cha mapambano, ukiwa pia ni msingi wa kistratijia uliobainishwa katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, ni msamiati jumla na uliokamilika, unaojumuisha ndani yake vipengele tofauti vya "kisiasa, kiutamduni, kiuchumi na kijeshi"; na "Uhuru", ni msamiati ambao siku zote huambatana na kifafanuzi, ambapo katika jamii ya Kiislamu maana yake ni "Uhuru ulio halali kidini". Shahidi madhlumu Ayatullah Beheshti ameifafanua nukta hiyo muhimu kwa kusema: "kulinda kwa uhalisia wake kujitawala kwa nchi, kunapatikana kwa kudumisha uadlifu na uhuru. Wakati uadilifu na uhuru unapokuwa haulindwi sawa sawa ndani ya jamii na nchi, huufungulia njia wenyewe ushawishi na satua ya maajinabi; na kinyume chake ni kuwa, kujitawala kwa taifa ndiko kunakoweza kuufanya uwe na maana halisi uhuru wa taifa hilo. Taifa ambalo katika moja ya hali zake, mathalani ya kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa, ni tegemezi kwa wengine, huwa limepoteza uhuru wake".

Rais Hassan Rouhani akisalimiana na umati wa wananchi katika maadhimisho ya miaka 30 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Tunapolidurusu faili la miaka 39 ya Mapinduzi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu tunadhihirikiwa na ukweli huo, kwamba taifa la Iran limeweza kwa heshima na fahari kubwa kusimama imara kukabiliana na njama, kuanzia za vita vya mtutu wa bunduki, vikwazo mpaka vita laini.

Katika kipindi cha miaka yote ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, maadui wa Iran wametumia nguvu za mabavu na mbinu laini kwa upande wa kijeshi na kiuchumi dhidi ya mapinduzi ya wananchi wa Iran; lakini mashinikizo yote hayo hayajaweza kupunguza hata chembe ndogo ya thamani ya mapinduzi hayo. Hatua kubwa zilizopigwa na taifa la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi, zimeweza kwa hakika kuvuruga na kusambaratisha mahesabu yote waliyojipangia maadui.

Wananchi katika maandamano ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kwa mtazamo wa wachambuzi, leo hii Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uthabiti mkubwa zaidi kuliko wakati wowote ule; na kama kabla ya hapo, maadui wa Mapinduzi walikuwa wakifanya kila njia kupotosha ukweli kuhusu Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, hivi sasa wamelazimika kukiri kwamba, ukweli hauwezi kufichika milele. Kwa sababu hiyo, Bahman 22 si kumbukumbu ya maadhimisho ya Mapinduzi tu, lakini pia ni alama ya ukweli, kwamba leo hii Mapinduzi ya Kiislamu yanasonga mbele katika njia ya ustawi na utukukaji; na yangali yameshikamana na tunu na thamani zake, pasi na kurudi nyuma hata masafa ya shubiri moja katika malengo yake matukufu ya kimapinduzi. Katika kipindi cha miaka 39 iliyopita, maadui wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wamepanga na kutekeleza njama mbalimbali ili kuukana mfumo huo, kuwavunja moyo wananchi na kuutia doa msingi wa kujitawala taifa la Iran. Lakini licha ya hatua na harakati hasi zote hizo hawajaweza kuidhuru na kuihasiri misingi ya Mapinduzi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu Imam Khomeini (kulia) na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei (kushoto)

Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umejengwa juu ya msingi wa kutoridhia kumnyongesha yeyote, wala kukubali kunyongeshwa na yeyote yule na kutetea haki zake mbele ya madola ya kibeberu duniani. Kwa sababu hiyo mfumo huu huru wa utawala unaotetea kujitawala wananchi wenyewe umeuchukiza na kuukasirisha Uistikbari wa dunia. Kwa kutegemea kura na irada ya wananchi wa Iran, Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umeyathibitishia mataifa yanayopigania kujitawala kwa maana yake halisi, kwamba  inawezekana kuwa ngangari mbele ya uchu na hulka ya kutotosheka ya maadui, kuifikia maana halisi ya uhuru na kujitawala na kutetea matakwa halali ya taifa. Nukta zote hizi ni vielelezo vya uendelevu na uwezo mkubwa wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, ambavyo vimejenga matumaini juu ya mustakabali kwa mataifa yanayopigania kuwa na uhuru wa kweli wa kujitawala na hivyo kuwa chachu kwao ya kusimama imara kukabiliana na ubabe na mabavu ya madola yenye nguvu duniani.../ 

 

 

Tags