Iran na Zimbabwe kushirikiana katika sekta ya afya
Mawaziri wa afya wa Iran na Zimbabwe wamesisitiza kuhusu kutekelezwa mapatano yaliyotiwa saini.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IRIB, Daktari Hassan Qadhizadeh Hashemi Waziri wa Afya wa Iran na mwenzake wa Zimbabwe Daktari David Parirenyatwa walibainisha hayo katika mkutano wao mjini Tehran Jumatatu usiku. Mawaziri hao wamebainisha kuhusu uhusiano wa nchi mbili katika uwekezaji na mafunzo katika sekta ya afya.
Waziri wa afya wa Iran amesema: "Ninanjitahidi kushawishi sekta binafsi za Iran kuwekeza nchini Zimbabwe."
Daktari Qadhizadeh ameongeza kuwa, tunatarajia kuwa Zimbabwe itasajili dawa za Iran ili zitumike kwa wingi nchini humo na pia kuuzwa katika nchi zingine za Afrika.
Aidha amesema vyuo vikua vya Iran viko tayari kushirikiana katika kutoa mafunzo kwa wataalamu na madaktari bingwa nchini Zimbabwe.
Kwa upande wake waziri wa afya wa Zimbabwe ameshangazwa na ustawi mkubwa wa Iran katika sekta za uzalishaji dawa. Amesema Zimbabwe iko tayari kushirikiana na Iran katika uzalishaji dawa. Aidha ameelezea matumaini yake kuhusu kutekelezwa mikataba ya utengenezaji dawa baina ya Iran na Zimbabwe.