SEPAH: Tutafanya juu chini kuwasaidia Wapalestina
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH sanjari na kulaani mauaji ya Wapalestina 17 waliokuwa wakiandamana kwa amani Ijumaa ya juzi katika mpaka wa Gaza ili kuadhimisha Siku ya Ardhi, limesema litafanya kila liwezekanalo kuwasaidia Wapalestina wapate haki zao.
Katika taarifa yake, SEPAH imeitaja Marekani na nchi za Ulaya kuwa ndio wahusika wakuu wa ukatili huo unaolenga kuubakisha hai utawala wa Kizayuni, ambao unavuta pumvi zake za mwisho.
Kadhalika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran limezilauma tawala vibaraka katika eneo hili la Mashariki ya Kati, kutokana na tabia zao za kuwa na uhusiano wa kisiri na kidhahiri na utawala haramu wa Israel.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, kuendelea kukingiwa kifua Israel hakutazaa matunda yoyote ya maana na badala yake, muqawama na mapambano ya wananchi yatazidi kushika kasi, na hatimaye kung'oa mzizi wa saratani (Utawala wa Kizayuni).
Vile vile Sepah imeitaka jamii ya kimataifa na watetezi wa kweli wa haki za binadamu kuchukua hatua za haraka za kukomesha kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina, badala ya kupiga domo tupu lisilo na faida yoyote.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi na Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Dk Ali Larijani ni miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu wa Iran waliotoa taarifa za kulaani ukatili huo wa jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina.