Velayati: Mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria yatajibiwa
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika Masuala ya Kimataifa amesema kuwa jinai iliyofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya kituo cha anga cha T-4 nchini Syria hayatapita hivihivi bila ya kujibiwa.
Dokta Ali Akbar Velayati ambaye yuko safarini mjini Damascus amesema kuhusu shambulizi lililofanywa na Israel dhidi ya kituo hicho cha anga kwamba, maadui wa Umma wa Kiislamu wanapaswa kuelewa kwamba, mashambulizi kama hayo ya kuvizia ni alama ya udhaifu wao na hayawezi kupita hivihivi bila ya kupewa jibu kali.
Itakumbukwa kuwa Jumatatu afajiri uwanja wa ndege za kijeshi wa T-4 ulioko katika mkoa wa Homs nchini Syria ulishambuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Waziri wa Vita wa Israel, Avigdor Lieberman amekiri katika mazungumzo yake na gazeti la Haaretz kwamba utawala huo umehusika na shambulizi hilo.
Mshauri wa Kiongozi Mkuu wa Iran katika Masuala ya Kimataifa ameashiria pia tuhuma zinazotolewa na Marekani dhidi ya Syria kwamba imefanya mashambulizi ya silaha za kemikali katika eneo la Douma huko Ghouta Mashariki na kusema: Miaka kadhaa iliyopita serikali ya Syria ilikabidhi silaha zake zote za kemikali kwa taasisi husika za kimataifa na maghala yake yote ya silaha hizo yamekaguliwa na taasisi hizo zilizothibitisha kwamba, Syria haimiliki silaha za aina hiyo.
Madai hayo ya Marekani na washirika wake yametolewa baada ya jeshi la Syria kupata ushindi mkubwa dhidi ya makundi ya kigaidi huko Ghouta Mashariki. Wachambuzi wa mambo wanasema madai hayo yametolewa kwa shabaha ya kuhafifisha na kufunika ushindi na mafanikio hayo.