Apr 17, 2018 08:01 UTC
  • Spika Larijani ataka kuimarishwa uhusiano wa kibiashara wa Iran na Vietnam

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhusiano wa kibiashara wa Iran na Vietnam unapaswa kustawishwa kama ulivyo uhusiano wa kisiasa kati ya nchi mbili hizo.

Dakta Ali Larijani, alisema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake huko mjini Haoni na Nguyễn Xuân Phúc Waziri Mkuu wa Vietnam ambapo sambamba na kusisitiza kwamba, daima uhusiano wa nchi mbili hizo umekuwa wa kirafiki na kuheshimiana pande mbili aliongeza kuwa, katika mwaka wa 45 wa uhusiano wa Hanoi na Tehran kuna haja ya kustawishwa zaidi ushirikiano kati ya nchi mbili hizi. 

Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa, kuna fursa nzuri kati ya pande mbili katika uga wa usafiri na uchukuzi wa baharini ambayo inaweza kuwa chachu ya kuongezwa ushirikiano baina ya Iran na Vietnam.

Dakta Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran

Kwa upande wake Nguyễn Xuân Phúc Waziri Mkuu wa Vietnam amesisitiza kwamba, serikali yake inaheshimu mno na kulipa kipaumbele suala la kuimarisha uhusiano wake mkongwe na Iran.

Amesema kwamba, nchi yake inataka Iran na Vietnam ziongeze kiwango cha mabadilishano ya kibiashara.

Aidha Nguyễn Xuân Phúc amesisitiza kwamba, Tehran na Hanoi zinapaswa kustawisha ushirikiano wao katika uga wa nishati, mawasiliano, ushirikiano wa kibenki, utalii na biashara.

Dakta Ali Larijani, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifajiri ya jana aliwasili Hanoi, mji mkuu wa Vietnam kwa safari rasmi ya kikazi ambapo lengo la safari hiyo ni kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo ili kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Tags