Apr 06, 2016 07:40 UTC
  • Iran yakosoa nchi zenye silaha za nyuklia kwa kukiuka mpatano

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amebainisha wasiwasi wake kuhusu mchakato wa kuangamiza silaha za nyuklia duniani.

Gholam Mohsen Dehqani, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa akizungumza Jumanne katika kikao cha Kamati ya Kuangamiza Silaha ya Umoja wa Mataifa amesema: "Hakuna maendeleo yoyote ya maana yaliyoshuhudiwa katika utekelezwaji wa mapatano ya kuangamiza silaha za nyuklia."

Amesema hivi sasa nchi kama vile Uingereza na Marekani zimetenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuimarisha maghala ya silaha hatari za nyuklia. Amebainisha kuwa Marekani imetenga bajeti ya dola trilioni moja kwa ajili ya kuunda silaha mpya za nyuklia.

Kuhusu mikakati ya kuwepo eneo la Mashariki ya Kati lisilo na silaha za nyuklia, Dehqani amesema: "Utawala wa Kizayuni wa Israel ndio kizingiti pekee cha kufikiwa lengo hilo." Aidha balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameashiria siasa za kiundumakuwili za baadhi ya madola makubwa yenye silaha za nyuklia na kusema,"Kuwepo silaha za nyuklia mikononi mwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni natija ya sera kama hizo."

Tags