Rais Rouhani: Iran itaendelea kuwa pamoja na Qatar
(last modified Mon, 18 Jun 2018 15:25:13 GMT )
Jun 18, 2018 15:25 UTC
  • Rais Rouhani: Iran itaendelea kuwa pamoja na Qatar

Rais Hassan Rouhani amekaribisha kustawishwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Qatar na kusisitiza kuwa hakuna kizuizi chochote cha kuzuia kustawishwa uhusiano huo na kwamba Tehran itaendelea kuwa pamoja na Doha.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Amir wa Qatar Sheikh Tamim Bin Hamad Al Thani, na kubainisha kuwa muqawama na kusimama imara wananchi na serikali ya Qatar katika kukabiliana na mashinikizo, vitisho na mzingiro wa kionevu kunastahili pongezi. Dakta Rouhani ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mzingiro iliobebeshwa Qatar ni wa kionevu na utasababisha mfarakano na mvutano zaidi kati ya nchi za eneo.

Huku akisisitiza kuwa sera za Tehran ni za kufikia maelewano na kufanya mazungumzo na nchi za eneo kwa ajili ya kutatua hitilafu, Rais Rouhani amesema, kufanywa juhudi za kuleta uthabiti na usalama katika Mashariki ya Kati ni kwa manufaa ya nchi zote za eneo hili na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitakidi kwamba sera za kuzusha chokochoko za baadhi ya nchi za eneo si sahihi; na kuendelea kwa mwenendo huo kutashadidisha matatizo yaliyopo katika nchi za eneo yakiwemo ya Palestina, Syria na Yemen.

Waislamu, wakiwemo watoto, wanaendelea kuteseka katka nchi za Yemen, Palestina, Syria, Libya, Somalia na kwengineko

Katika mazungumzo hayo , Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametanabahisha pia kwamba mgogoro wa Yemen hauwezi kutatuliwa kwa nguvu za kijeshi na kueleza kuwa hujuma za karibuni dhidi ya bandari ya Al-Hudaydah zitasababisha maafa ya kibinadamu nchini Yemen. Rais Rouhani amesisitiza kwamba, kuendelea mapigano hayo kumewafanya wananchi masikini wa Yemen waelemewe na mashinikizo yasiyohimilika na kwamba ni jukumu la wote kuwasaidia wananchi hao madhulumu.

Kwa upande wake, Amir wa Qatar ameisifu na kuipongeza misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kadhia ya mzingiro iliowekewa nchi yake na kusisitiza kwamba Doha haitaisahau katu misimamo hiyo iliyochukuliwa na Tehran. Sheikh Tamin bin Hamad Al Thani aidha amebainisha kuwa: Qatar inatilia mkazo kutatuliwa hitilafu zote katika eneo kwa njia ya mazungumzo tu, na kwamba nchi yoyote ile haiwezi kulazimisha na kuitwisha mitazamo yake kwa nchi nyingine.../

Tags