Iran na Afrika zajadili fursa za ushirikiano wa kibiashara baina yao
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i47127-iran_na_afrika_zajadili_fursa_za_ushirikiano_wa_kibiashara_baina_yao
Kikao cha kujadili fursa za kibiashara kati ya Iran na Afrika kimefanyika hapa mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na mabalozi wa nchi za Kenya, Algeria, Ivory Coast, Mauritania na Ghana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 30, 2018 23:43 UTC
  • Iran na Afrika zajadili fursa za ushirikiano wa kibiashara baina yao

Kikao cha kujadili fursa za kibiashara kati ya Iran na Afrika kimefanyika hapa mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na mabalozi wa nchi za Kenya, Algeria, Ivory Coast, Mauritania na Ghana.

Akizungumza pembeni ya kikao hicho, Hassan Khosrujerdi, mkuu wa baraza la ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Afrika amesema: Kwa sasa kiwango cha bidhaa za Iran zinazosafirishwa kupelekwa katika nchi za Afrika ni zenye thamani ya karibu dola bilioni tatu na milioni 700, ambapo bidhaa zenye thamani ya dola milioni 700 zinasafirishwa moja kwa moja kuelekea nchi za Afrika na zilizosalia zinasafirishwa kupitia nchi za kusini mwa Ghuba ya Uajemi zikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Oman.

Khosrujerdi amesema uhamishaji wa malipo ni moja ya matatizo yanayoukabili ubadilishanaji wa kibiashara kati ya Iran na nchi za Afrika na kuongeza kwamba ubadilishanaji bidhaa ni njia bora ya kukabiliana na kizuizi hicho.

Akizungumza katika kikao hicho, balozi wa Kenya mjini Tehran Bi Rukia Subow ameashiria kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kueleza kwamba: jibu la Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa hatua hiyo ya Marekani limeleta matumaini; na uchukuaji hatua wa aina hiyo umekaribishwa na jamii ya kimataifa.

Bi Subow aidha amekaribisha wazo la kubadilishana bidhaa kati ya nchi za Kiafrika na Iran.

Tangu miaka kadhaa iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikilipa kipaumbele suala la kustawisha uhusiano na nchi za Afrika; na hadi sasa zimeshafanywa safari za jumbe nyingi za kiuchumi na kisiasa kati ya pande mbili.../