Meja Jenerali Bagheri: Maadui ni walowezi Ghuba ya Uajemi
(last modified Thu, 30 Aug 2018 02:26:12 GMT )
Aug 30, 2018 02:26 UTC
  • Meja Jenerali Bagheri: Maadui ni walowezi Ghuba ya Uajemi

Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kutokana na uimara wa kikosi cha majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH), nchi maadui huwa zina woga mkubwa kabla ya kuingia katika Lango Bahari la Hormoz (la kusini mwa Iran) na katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, maadui hao wamelazimika kuheshimu sheria za kimataifa.

Mtandao wa habari wa Sepah News umemnuku Meja Jenerali Mohammad Bagheri akisema hayo katika kongamano la 21 la makamanda, maafisa na wakurugenzi wa Iran nzima wa kikosi cha majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lililofanyika mjini Mash'had (kaskazini mashariki mwa Iran) na kusisitiza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Iran kamwe havidharau vitisho vyovyote vile vya adui na inabidi kuimarisha nguvu zetu za kuzuia mashambulizi, kama njia bora ya kupambana na adui.

Lango Bahari la Hormoz

 

Mkuu huyo wa vikosi vya ulinzi vya Iran pia amesema, Tehran daima iko macho na inafuatilia kila mkakati mpya wa adui. Amefafanua zaidi kwa kusema, nchi maadui kama zitachupa mipaka na kutoka nje ya mstari wa haki zao kwa mujibu wa sheria za kimataifa katika Lango Bahari la Hormoz, basi Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH halitasita hata kidogo kuzichukulia hatua.

Vile vile amesisitiza kuwa, Ghuba ya Uajemi ni nyumbani na ndio watani na mahala pa asili pa kuishi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hivyo maadui waliojileta kwenye eneo hili ni walowezi. Aidha amesema, maadui wanapawaswa kutambua vyema kuwa, Ghuba ya Uajemi si mahala pazuri kwao kwa ajili ya vita na mapigano kwani hata wataalamu wao wanasema kuwa, hawana uwezo wa kukabiliana na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu.