Russia yaitaka IAEA kutoa dhamana ya utekelezaji wa JCPOA
Russia imeutaka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) itoe dhamani ya utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Makubaliano hayo yalitiwa saini mwezi Juni mwaka 2015 mjini Vienna Austria baina ya Iran kwa upande mmoja na kundi la 5+1 linajumuisha nchi za Uingereza, Ufaransa, Marekani, Russia, China na Ujerumani kwa upande wa pili. Makubaliano hayo yalianza kutekelezwa mwezi Januari 2016.
Russia ambao ni mwanachama wa kundi la 5+1 daima imekuwa ikitilia mkazo suala la kulindwa na kutekelezwa makubaloano hayo ya nyuklia. Hivyo, kwa kutilia maanani hatua ya Marekani ya kuweka tena vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran na jitihada za Washington za kutaka makubaliano hayo yavunjwe, Moscow imechukua hatua mpya na kuutaka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki udhamini utekeleza wake endelevu. Mwakilishi wa Russia katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia, Mikhail Ulyanov alisema jana katika kikao cha Baraza la Magavana wa IAEA mjini Vienna kwamba: Inatarajiwa kuwa Wakala Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia utatekeleza majukumu yake kama refa na mwamuzi asiyependelea upande wowote na kujenga msingi imara wa kuendelea utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Russia itaendeleza juhudi zake za kuhakikisha makubaliano ya nyuklia ya Iran ambayo yanadhamini maslahi ya jamii yote ya dunia, yanaendelea kutekeleza."
Misimamo na ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia ambao ndiyo taasisi ya kiufundi na chombo cha kimataifa cha kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA, vimeifanya Marekani ikate tamaa ya kupata visingizo vya kuiwekea mashinikizo zaidi Iran na sasa imeelekeza mazingatio yake kwenye masuala na madai yasiyo na msingi na yasiyo na uhusiano na makubaliano ya nyuklia kama vile miradi ya makombora ya Iran na nafasi na ushawishi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati.
Tarehe 8 Mei mwaka huu Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kujiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuanza tena vikwazo dhidi ya Iran. Hatua hiyo ilikoselewa na kupingwa sana kote duniani hususan na nchi wanachama wa kundi la 5+1. Katika mkondo huo Russia inaamini kuwa, kufutwa makubaliano hayo ya nyuklia kutakuwa na taathira nyingi mbaya kwa amani na usalama wa duniani na kwa sababu hivyo maafisa wa ngazi za juu wa Russia wamekuwa wakitoa wito wa kulindwa na kuendelea kutekelezwa makubaliano hayo. Wakati huo huo uhasama wa Marekani wa kuanzisha tena vikwazo dhidi ya Iran umekabiliwa na upinzani mkubwa wa kimataifa na nchi nyingi zikiwemo Russia, China na Uturuki zimetangaza kwamba, hazitafuata takwa la Marekani la kuisusia Iran. Russia inasema Marekani inapaswa kutafuta njia nyingine za kutatua hitilafu zake na Iran na si kuvuruga makubaliano ya kimataifa ya JCPOA. Rais Vladimir Putin wa Russia anasema: "Moscow inaamini kwamba, makubaliano ya JCPOA ni wenzo ambao unarahisisha kuzuia uwepo wa silaha za nyuklia husuan katika eneo la Mashariki ya Kati; hivyo hapana budi kulindwa wenzo huo."
Licha ya misimamo hiyo ya Russia na nchi nyingine wanachama wa kundi la 5+1 kuhusu udharura wa kulindwa makubaliano ya nyuklia ya Iran lakini Donald Trump angali anapiga ngoma za kutaka yavunjiliwe mbali. Hata hivyo kiongozi huyo wa Marekani ameshindwa kuzishawishi nchi za dunia kuungana na Washington na sasa anatumia mabavu na vitisho kwa ajili ya kufikia malengo yake, suala ambalo linaifanya Marekani itengwe zaidi katika uga wa kimataifa.