Iran yatoa onyo kali kwa watawala mafashisti wa Israel
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amewatahadharisha viongozi wabaguzi, maghururi na wasio na mantiki wala adabu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu athari mbaya za lugha yao chafu, isiyo na mantili na vilevile fikra zao kuhusiana na taifa kubwa la Iran.
Bahram Qassemi ambaye alikuwa akijibu matamshi ya jeuri na yaliyojaa chuki na vinyongo ya Rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Reuven Rivlin kuhusiana na taifa la Iran amesema: Viongozi wenye fikra potofu na sifa za kishetani wa Israel ambao wamekuwa wakifanya mikakati ya kuwatenganisha Wairani na serikali yao hawawezi tena kudhibiti ndimi zao na sasa wamejitokeza na lugha ya matusi na jeusi na kutoa maneno yanayogongana na kukinzana kuhusiana na Wairani na kujichoma wenyewe katika chuki na vinyongo vyao.
Bahram Qassemi ameongeza kuwa, ni jambo la kutia aibu na fedheha kubwa kwa viongozi wa utawala unaosifika kwa ukatili, mauaji, udhalili na laghai kama Israel kusema kwamba "kuna ulazima wa kulitia kwenye njaa taifa la Iran" ambalo ni taifa lenye historia ya siku nyingi, shujaa na lenye utamaduni mkongwe ambalo liliokoa kaumu ya Mayahudi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, taifa kubwa na lenye ustaarabu la Iran sambamba na kuheshimu haki za wafuasi wa dini ya Nabii Mussa Kalimullah (as), linawatambua kuwa ni tofauti na watawala mafashisti, wavamizi wa utawala ghasibu unaoikalia Palestina kwa mabavu.
Akiwa pamoja na Kansela wa Ujerumani katika mji mtakatifu wa Quds, siku ya Alkhamisi iliyopita Rais wa Israel, Reuven Rivlin alitoa matamshi ya dharau dhidi ya taifa la Iran akisema: "Kuna ulazima wa kulitia katika njaa taifa la Iran".