Kongamano la Mazungumzo ya Tamaduni za Iran na Afrika lafanyika A. Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i48971-kongamano_la_mazungumzo_ya_tamaduni_za_iran_na_afrika_lafanyika_a._kusini
Kongamano la Mazungumzo Baina ya Tamaduni za Iran na Afrika limefanyika leo Pretoria nchini Afrika Kusini likiwashirikisha wanafikra wa Kiafrika.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 22, 2018 12:53 UTC
  • Kongamano la Mazungumzo ya Tamaduni za Iran na Afrika lafanyika A. Kusini

Kongamano la Mazungumzo Baina ya Tamaduni za Iran na Afrika limefanyika leo Pretoria nchini Afrika Kusini likiwashirikisha wanafikra wa Kiafrika.

Balozi wa Iran nchini Afrika Kusini, Muhsin Muwahidi Qummi ambaye amehutubia kongamano hilo amesema kuwa, Iran inayopinga ubeberu na tabia ya kukubali ubeberu, inafanya jitihada za kuwa na uhusiano na nchi huru na zinazojitawala na kwamba, kuwa na uhusiano mwema na nchi za Afrika ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu Iran.

 Muwahhidi Qummi ameongeza kuwa, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilikata uhusiano wake na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na kuanzisha mawasiliano na makundi ya wapigania uhuru kutokana na misimamo na sera zake za kuwaunga mkono na kuwasaidia watu wanaodhulumiwa kote duniani; na baada ya kung'olewa utawala wa ubaguzi wa rangi ilianzisha tena uhusiano wake na Afrika Kusini. 

Cheryl Hendricks Mkuu wa Kitendo cha Utafiti wa Sayansi za Jamii nchini Afrika Kusini ameashiria uwezo mkubwa wa Iran na kusema kwamba, udiplomasia wa utamaduni una mchango mkubwa katika kuzikurubisha pamoja nchi mbalimbali. 

Mkurugenzi Mkuu wa kitengo cha utafiti cha Wizara ya Utamaduni ya Afrika Kusini, Karen Sodin ambaye pia amehutubia kongamano hilo amesema kuwa, uhusiano wa nchi yake na Iran ni mkubwa na wenye historia ya muda mrefu na ametoa wito wa kupanuliwa zaidi ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali.

Kongamano la Mazungumzo Baina ya Tamaduni za Iran na Afrika limehudhuriwa pia na wasomi na wanafikra kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Zimbabwe, Botswana na mwenyeji Afrika Kusini.