Mazoezi ya kijeshi kusini mashariki mwa Iran
(last modified Wed, 13 Apr 2016 04:18:00 GMT )
Apr 13, 2016 04:18 UTC
  • Mazoezi ya kijeshi kusini mashariki mwa Iran

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) linaendelea na mazoezi makubwa ya kijeshi katika eneo la kusini mashariki mwa nchi.

Luteka hiyo iliyopewa jina la Mtume Mtukufu SAW imeanza Jumanne katika mkoa wa Sistan na Baluchestan ambapo pia kumezinduliwa ndege mpya isiyo na rubani au drone ilioyotengenezwa hapa nchini na yenye uwezo mkubwa.

Drone hiyo ijulikanayo kama Hamasa inatumika kwa mara ya kwanza katika mazoezi ya jeshi baada ya uundwaji wake kutangazwa miaka miwili iliyopita. Drone hiyo ina uwezo mkubwa wa kazi za upelelezi na kurusha makombora mbali na kuwa na uwezo wa kuruka juu sana. Drone zingine zilizotengenezwa nchini Iran zinazotumika katika luteka hiyo ni pamoja na Mohajer, Ababil na Shahed.

Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha IRGC Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour amesema mazoezi hayo ya siku tatu yatafanyika pia katika mikoa ya Kerman, Khorasan Kusini na Hormozgan.

Hivi karibuni pia vikosi vya ulinzi vya Iran vilifanya mazoezi na kufanyia majaribio zana za kisasa za kujihami. Machi 9 IRGC ilifanyia majaribio yaliyofana makombora mawili ya balistiki ya Qader-H na Qader-F. Machi nane pia Iran ilifanya majaribio yaliyofana ya kombora la Qiam.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa uwezo wake mkubwa wa kijeshi si tishio kwa nchi yoyote bali ni kwa ajili ya kujihami.

Tags