Bahram Qassemi: Wananchi wa Iran watazishinda siasa za ubabe na utumiaji mabavu
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, wananchi wa Iran wataushinda ubabe na utumiaji mabavu kutoka upande wowote ule, na historia ni ushahidi wa wazi wa utamaduni na mwenendo huu wa Wairani.
Bahram Qassemi amebainisha kuwa, Marekani inafanya kila iwezalo ili kuwakwamisha na kuwaudhi Wairani na kuongeza kuwa, Washington inadhani kwamba, kwa kufanya mambo bila ya busara, kutumia uongo na hadaa itaweza kudhoofisha umoja na mshikamano wa wananchi wa Iran.
Qassemi ameeleza kwamba, Wairani wanaitambua Marekani kama dola halifu, haramia na vamizi.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, utendaji na mwenendo wa Marekani ni wa 'karne za kati' na kubainisha wazi kwamba, washauri wa ikulu ya Marekani White House wanaota ndoto za alinacha na hali ya kupenda makuu na hili ni jambo ambalo limewapelekea wafanye makosa mtawalia.
Bahram Qassemi ameashiria matamshi ya Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia aliyesema kuwa, ulimwengu unapaswa kujikita zaidi katika kile alichokiita 'tishio la Iran na Uturuki' na kubainisha kwamba, Wasaudia wanafanya makosa na muda si mrefu watajuta.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran sambamba na kubainisha kwamba, Israel ina sera za wazi za kuzusha mizozo katika Ulimwengu wa Kiislamu ameeleza kuwa, safari ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel katika nchi za Kiarabuu ni njama za kuleta mifarakano baina ya madola ya Kiarabu na Kiislamu.