Kiongozi Muadhamu: Umma wa Kiislamu unapaswa kuwa na umoja na mshikamano
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49756-kiongozi_muadhamu_umma_wa_kiislamu_unapaswa_kuwa_na_umoja_na_mshikamano
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa umoja, mshikamano na kauli moja ya ulimwengu wa Kiislamu vitazishinda njama za maadui.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Nov 25, 2018 17:20 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Umma wa Kiislamu unapaswa kuwa na umoja na mshikamano

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa umoja, mshikamano na kauli moja ya ulimwengu wa Kiislamu vitazishinda njama za maadui.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo alipokutana na viongozi wa nchi na wageni wanaoshiriki Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu na watu wa matabaka mbalimbali. Amewahutubu wanafikra na maulama wa kidini amesema; "Fanyeni kila muwezalo kuimarisha mwamko wa Kiislamu na muqawama katika eneo la  Mashariki ya Kati kwani njia pekee ya kuliokoa eneo hili ni kueneza moyo na fikra hii."

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameashiria wasiwasi wa madola ya kibeberu kuhusu mwamko wa mataifa ya Kiislamu na kusema kuwa, mahala popote ambapo Uislamu unadhibiti mioyo ya watu, ubeberu husambaratishwa na kwa mara nyingine mwamko wa Kiislamu katika eneo hili utatoa kipigo kwa ubeberu huo. Kadhalika ameashiria baadhi ya nchi za eneo hili ambazo badala ya kufuata mafundisho ya Uislamu na Qur'ani, zinaifuata Marekani na kusema: Kwa kuzingatia dhati yake ya kibeberu, Marekani inazidhalilisha nchi hizo, na kama ambavyo kila mtu ameshuhudia, Rais mpayukaji wa Marekani amewafananisha watawala wa Saudia  na "ng'ombe anayekamuliwa maziwa".

Baadhi ya maulama wa ulimwengu wa Kiislamu waliofika kumzuru Kiongozi Muadhamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja udhalilishaji huo wa Rais wa Marekani kuwa unaowavunjia heshima raia wa Saudia na wa mataifa ya Waislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kwamba, baadhi ya watawala wa nchi za Kiislamu wanafanya jinai dhidi ya Wapalestina na Wayemeni kwa kushirikiana na Marekani na kwamba, hata hivyo wananchi madhlumu wa Palestina na Yemen wataibuka washindi na Marekani itafeli katika ndoto zake hizo.

Kadhalika amesema kuwa uwezo wa Marekani na utawala haramu wa Israel katika eneo la Mashariki ya Kati umezidi kuwa dhaifu na kwamba, tangu Israel iliposhindwa na harakati ya Hizbullah katika vita ya siku 33 imeendelea kuporomoka ambapo miaka miwili iliyofuatia ilistahamili kwa siku 22 tu na katika vita na Wapalestina wa eneo la Ukanda wa Gaza haikuweza kustahmili isipokuwa kwa siku nane tu katika kukabiliana na muqawama. Ayatullah Khamenei amesema wiki iliyopita Israel haikuweza kustahamili mapigo ya wanamapambano wa palestina isipokuwa kwa muda wa siku mbili tu na kwamba kushindwa huko kunaonyesha udhaifu endelevu wa utawala huo khabithi wa Kizayuni.

Aidha ameashiria muqawama na mapambano ya miaka 40 ya wananchi wa Iran licha ya matatizo na mashinikizo yote na kusisitiza kwamba, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinakosea kwa kulitisha taifa la Iran.