Larijani: Walimwengu wajulishwe kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni
Ali Larijani Spika wa Bunge la Iran, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, amesema kuna haja ya kuwafahamisha walimwengu kuwa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ndio sababu ya kuunga mkono malengo matukufu ya Wapalestina.
Larijani ameyasema hayo Jumamosi mjini Tehran wakati alipokutana na wabunge kadhaa wa Palestina ambapo amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuwaunga mkono Wapalestina.
Aidha amesema nchi zote za eneo la Mashariki ya Kati na duniani zinapaswa kuzidisha uungaji mkono wao kwa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina.
Mahmoud Al Zahar ambaye ameongeza ujumbe huo wa wabunge Wapalestina mjini Tehran ameishukuru kwa dhati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuendelea kuwaunga mkono watu wa Palestina.
Al Zahar ambaye pia ni kati ya waanzilishi wa harakati ya kupigania ukombozi wa Palestina ya Hamas, amesisitiza kuwa, kadhia ya Quds (Jerusalem) imewakutanisha pamoja wapenda uhuru kote duniani.Al Zahar pia amemwalika Spika wa Bunge la Iran kutembelea Ukanda wa Ghaza.
Wapalestina wanapigania ukombozi wa ardhi zao ambazo zinaendelea kukaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel.