Meja Jenerali Safavi: Marekani haina nafasi tena Mashariki ya Kati
Msaidizi na Mshauri mwandamizi wa Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Marekani haina nafasi tena katika eneo la Mashariki ya Kati na kwa msingi huo Wamarekani wanapaswa kuondoa katika eneo hili.
Meja Jenerali Sayyid Yahya Rahim Safavi amesema hayo hii leo katika hafla ya kiutamaduni iliyofanyika mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa nchi na kuongeza kuwa, Marekani ilifanya makosa makubwa na ya kistarajia ya kuanzisha kampeni za kijeshi Magharibi mwa Asia, na kitendo chake hicho kimepelekea kuuawa maelefu ya wanajeshi wake katika nchi za Afghanistan na Iraq.
Meja Jenerali Safavi ameashiria hotuba ya mwezi Juni mwaka huu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, aliposema kuwa Rais Donald Trump wa Marekani alikiri binafsi kuwa nchi hiyo imetumia dola trilioni 7 katika eneo la Magharibi mwa Asia pasina kufanikiwa kufikia malengo yake ghalati.
Huku akizitaja Iran, China, India na Russia kuwa mataifa mapya yenye nguvu kubwa upande wa mashariki katika zama hizi, Mshauri huyo wa Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Ali Khamenei amebainisha kuwa, utamaduni wa Kiislamu na Ustaarabu wa Iran umesimama kidete dhidi ya Uliberali wa Marekani.
Aidha amesema bayana kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mhimili wa muqawama Mashariki ya Kati ambapo imeikwamisha Marekani na kuifanya ishindwe kuunda Mashariki ya Kati mpya na hivyo kulazimika kuondoka huko Syria.
Amesema kuwa, mustakabali wa Mashariki ya Kati umo mikononi mwa mataifa ya eneo hili, na Marekani haina nafasi yoyote.