Iran: Kuwepo Marekani katika Ghuba ya Uajemi kunasababisha wasiwasi na mivutano
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Tokea awali sisi tumekuwa tukiamini kwamba kuwepo Marekani katika Ghuba ya Uajemi, mbali na kuwa ni kinyume cha sheria lakini pia kunasababisha hali ya wasiwasi na mivutano."
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na kanali ya televisheni ya Phoenix ya China.
Zarif amefafanua kuwa kuwepo manowari za Marekani katika Ghuba ya Uajemi, badala ya kuwa na taathira chanya, kunasababisha mivutano na hali ya wasiwasi; na kila Marekani inapozidisha kiwango cha uwepo wake katika Ghuba ya Uajemi, nchi zote za eneo hili zimekuwa zikikabiliwa na hatari.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: "Iran ni nchi yenye nguvu na inao uwezo wa kulinda maslahi yake; na eneo ndilo linaloweza kudhurika kwa kuwepo Marekani; na ni baidi kwa Marekani kuwa katika nafasi ya kuweza kuitisha Iran.
Kuhusu kuondoka vikosi vya jeshi la Marekani nchini Syria, Dakta Zarif amesema: "Sisi bado hatujajua Marekani ina mpango gani; lililo muhimu kwetu ni kwamba siasa za Marekani katika eneo ni siasa hatari na inapasa zibadilishwe."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amesema: "Hamu ya Iran ya kuwa na uhusiano na China ni ya malengo ya kistratejia, si ya kimbinu na ya muda maalumu; na China ni rafiki wa kuaminika kwa Iran; hivyo ninachotaka, China nayo iwe na uhakika wa jambo hilo".../