Zarif: Iran haitazisubiri nchi za Ulaya
(last modified Tue, 08 Jan 2019 07:42:48 GMT )
Jan 08, 2019 07:42 UTC
  • Mohammad Javad Zarif
    Mohammad Javad Zarif

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, Tehran inafanya mazungumzo na washirika wake wa jadi kwa ajili ya kudhamini maslahi ya watu wa Iran.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo mapema leo Jumanne mjini New Delhi alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa India, Nitin Gadkari. Akijibu swali kuhusu mchakato wa kubuni Mfumo Maalumu kwa Ajili ya Mabadilishano ya Kifedha na Iran, kwa Kiingereza Special Purpose Vehicle,(SPV), Zarif amesema: "Tehran itaendelea kushirikiana na nchi za Ulaya kuhusu SPV lakini haitazisubiri."

Zarif ameendelea kusema kuwa: "Nchi za Ulaya zinajitahidi kuhakikisha kuwa Iran inapata maslahi ya kiuchumi katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA  lakini hazijaweza kuchukua hatua iliyotarajiwa."

Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yuko safarini nchini India kwa ziara rasmi na leo amekutana na waziri wa uchukuzi wa nchi hiyo, Nitin Gadkari. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif  (kushoto) akiwa na Waziri wa Uchukuzi wa India Nitin Gadkari-New Delhi 08/01/2018

Leo asubuhi pia Zarif ameshiriki katika kikao ambacho kimefanyika katika Baraza la India la Masuala ya Dunia (ICWA) ambapo amebadilishana maoni na wasomi na wanafikra wa India kuhusu matukio ya hivi karibuni duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran jana Jumatatu alielekea India kwa lengo la kushiriki katika kongamano la kila mwaka la mazungumzo la Raisina.

Tags