Kiongozi Muadhamu: Wanafunzi wa vyuo vikuu ni tarajio la Jamhuri ya Kiislamu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba, kuungana wanavyuo wa Iran katika kuna zote za dunia na harakati ya maendeleo na kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isiyahitajie madola ya kigeni, ni mapambano ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo katika ujumbe wake uliosomwa leo na Hujjatul-Islam Javad Ejei katika kikao cha 53 cha Muungano wa Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu barani Ulaya kilichofanyika katika Kituo cha Kiislamu cha Hamburg, Ujerumani na kusema kuwa, wanafunzi wa vyuo vikuu ni miongoni mwa matarajio makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameongeza kwamba, jambo linalopaswa kujulikana kwa watu wote ni kwamba, hivi sasa kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu idadi kubwa ya wanafunzi wa jana wa vyuo vikuu wanafanya kazi kubwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na matunda ya uhudumu zao katika maendeleo ya elimu na teknolojia yanahisika kote nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba, wanafunzi wa vyuo vikuu katika pembe zote za dunia watakuwa na fursa ya kujiunga na makundi yanayotoa huduma ya vijana waumini na kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ijitosheleze na isiyategemee kabisa madola ya kiigeni. Amesisitiza kwamba harakati hiyo inapofanyika kwa ikhlasi na kutaka radhi za Mwenyezi Mungu huwa ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mkutano wa 53 wa kila mwaka wa Muungano wa Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu barani Ulaya umefanyika leo mjini Hamburg, Ujerumani katika Kituo cha Kiislamu cha mji huo.