Rais Rouhani: Iran haiogopi vikwazo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Iran haiogopi vikwazo na wala haitalegeza msimamo kuhusu malengo yake."
Rais Rouhani ameyasema hayo leo Jumanne katika kikao cha maafisa wa mkoa wa Golestan kaskazini mwa Iran na kuongeza kuwa, hivi sasa Iran iko katika vita vya kiuchumi. Amesema pande zinazokabiliana na Iran katika vita vya kiuchumi ni Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na tawala kadhaa za Ghuba ya Uajemi.
Rais Rouhani amebainisha kuhusu malengo ya Marekani katika vita vya kiuchumi dhidi ya Iran na kusema: "Kudhoofisha nafasi ya Iran katika eneo, kukabiliana na ustawi wa Iran katika uga wa makombora na nyuklia, kuweka vizuizi katika njia ya ustawi na kuchochea chuki baina ya wananchi na viongozi ni kati ya malengo ambayo Marekani inayafuatilia katika vita vya kiuchumi dhidi ya Iran lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaweza kupita kwa mafanikio katika kipindi hiki cha vita."
Rais wa Iran aidha amesistiiza kuwa, Iran haijawahi kuhujumu sheria za kimataifa na kuongeza kuwa: "Kinyume na Marekani ambayo imejiondoa katika mapatano ya JCPOA, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umetangaza kuwa Iran imefungamana kikamilifu na ahadi zake za kimataifa."

Rais Rouhani ameashiria kufeli Marekani na waitifaki wake katika eneo la Asia Magharibi na kuongeza kuwa: "Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, baadhi ya nchi za eneo zimenunua silaha zenye thamani ya dola bilioni 100 kutoka kwa Marekani lakini pamoja na kuwa na silaha hizo zimeshindwa katika vita vya Yemen."