Larijani: Mapinduzi ya Kiislamu ni mafanikio makubwa ya karne
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran, Bunge la Iran, amesema Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni mafanikio makubwa ya karne.
Ali Larijani ameyasema hayo Jumanne katika kikao chake na Kamati Kuu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Mwaka wa 40 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema kulinda Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kazi muhimu zaidi inayofuatiliwa na kamati hiyo.
Aidha, Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa: "Mapinduzi ya Kiislamu yamefika katika awamu ambayo adui ana hila na anatekeleza njama za kudhoofisha nafasi ya Mapinduzi."
Larijani amebaini kuwa, baadhi ya matamshi ya maadui dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ni ya kawaida sana na kuongeza kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu yaliuondoa madarakni utawala fisadi na kuleta serikali ya wananchi na haya si mafanikio madoko kwani nchi nyingi duniani zinakumbwa na tatizo hilo la serikali fisadi.
Amesema taifa la Iran lilifankiwa kuondoa madarakani utawala wa kidikteta na hivi sasa viongozi wote nchini wanachaguliwa kwa kura za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za wananchi.
Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa, maadui wa Iran wanafahamu kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni dola adhimu katika eneo ambalo haliwezi kuondolewa.