Rouhani: Maandamano ya Wairani tarehe 22 Bahman yatajibu njama za maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51378-rouhani_maandamano_ya_wairani_tarehe_22_bahman_yatajibu_njama_za_maadui
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mahudhurio makubwa ya wananchi wa Iran katika maandamano ya tarehe 22 Bahman (11 Februari) yatatoa jibu kali kwa njama zote za maadui.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 06, 2019 11:56 UTC
  • Rouhani: Maandamano ya Wairani tarehe 22 Bahman yatajibu njama za maadui

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mahudhurio makubwa ya wananchi wa Iran katika maandamano ya tarehe 22 Bahman (11 Februari) yatatoa jibu kali kwa njama zote za maadui.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo mjini Tehran baada ya kikao cha baraza lake la mawaziri. Amelipongeza taifa la Iran kwa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuwataka wananchi washiriki kwa wingi katika maandamano ya kuadhimisha mapinduzi hayo. Amesema kuwa, wananchi ndio wamiliki halisi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Rais Rouhani ameashiria njama zinazofanywa na maadui dhidi ya wananchi wa Iran na kusema: Katika mwaka mmoja uliopita maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu yaani Wamarekani na Wazayuni, wamefanya jitihada kubwa za kuwakatisha tamaa wananchi wa Iran kuhusiana na mustakbali. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, licha ya uadui huo wote, mahudhurio makubwa ya Wairani katika maandamano ya tarehe 11 Februari yatawaonesha walimwengu kwamba, wana matumaini mema kuhusu mustakbali wa nchi yao na wala hawajakata tamaa au kupoteza matumaini.

Rouhani amesema serikali mpya ya Marekani imekuwa ikizungumza na taifa la Iran kwa lugha siyo sahihi na kusema: Matatizo ya eneo la Mashariki ya Kati yanatokana na uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya nchi za eneo hilo na mataifa ya Mashariki ya Kati yanajua vyema kwamba, Iran daima imekuwa ikisaidia juhudi za kuimarisha amani na usalama wa eneo hili.

Rais Rouhani amesisitiza kuwa, Iran ni mhanga wa ugaidi lakini daima imekuwa ikipambana na ugaidi na leo hii sehemu kubwa ya usalama wa eneo hili inatokana na misaada na himaya ya Jamhuri ya Kiislamu kwa mataifa ya Mashariki ya Kati dhidi ya ugaidi.

Amesema sera za Marekani za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine haziishii katika eneo la Asia magharibi bali Wamarekani wanaingilia masuala ya America ya Latini kama huko Venezuela.