Zarif: Kuanzisha vita dhidi ya Iran ni sawa na kujitia kitanzi
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa jitihada za aina yoyote za kutaka kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran ni sawa na kujitia kitanzi na kujinyonga.
Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano yake na televisheni ya Marekani ya NBC katika Mkutano wa Usalama wa Munich nchini Ujerumani na kuongeza kuwa: Wale walioafiki kuanzishwa vita dhidi ya Iraq ndio hao hao wanaotaka kuanzisha vita dhidi ya Iran, lakini hatimaye wataelewa kuwa, kuingia vitani na Iran ni sawa na kujitia kitanzi.
Zarif amesema uhalali wa serikali nchini Iran unatokana na wananchi wenyewe na kuongeza kuwa, baadhi ya maafisa wa serikali ya Donald Trump huko Marekani wanafanya jitihada za kuanzisha vita dhidi ya Iran na hapana shaka watashindwa.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amepinga uwezekano wa aina yoyote wa kufanya mazungumzo na Marekani kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema kuwa: Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yamefikiwa baada ya mazungumzo ya miaka 13, sasa inawezekana vipi kufikia mapatano na Donald Trump ambaye hakubali wala kuamini makubaliano ya kimataifa?
Muhammad Javad Zarif ameashiria jinsi Marekani ilivyojiondoa katika makubaliano kadhaa ya kimataifa yakiwemo makubaliano ya silaha za nyuklia za masafa ya kati na Russia, kujiondoa nchi hiyo katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na kujiondoa kwake katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja huo na kusema kuwa, Iran kamwe haitafanya tena mazungumzo kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na haimwamini Rais Donald Trump wa Marekani ambaye haheshimu saini yake mwenyewe.