IRGC: Saudia ndiyo roho ya maovu yote Mashariki ya Kati
Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema Saudi Arabia ndiyo roho ya maovu yote katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kote kwa ujumla.
Brigedia Jenerali Hussein Salami amesema hayo leo katika kikao cha kuwakumbuka mashahidi waliouawa hivi karibuni katika shambulizi la kigaidi kusini mashariki mwa Iran na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu bila shaka italipiza kisasi cha damu ya mashahidi waliouawa katika hujuma iliyotokea katika mkoa wa Sistan na Baluchistan
Naibu Kamanda Mkuu wa IRGC amebainisha kuwa, Iran itachukua hatua za kukabiliana na njama za pande tatu za shari, yaani Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na vibaraka wao wa Kiarabu katika eneo hili.
Brigedia Jenerali Hussein Salami ameongeza kuwa, shambulizi hilo halikuwa tukio la kushtukiza, bali ni katika wimbi la stratejia hatari ya pande tatu hizo za shari linaloikabili dunia.
Ikumbukwe kuwa, Jumatano iliyopita ya Februari 13, basi lililokuwa limewabeba askari walinda mpaka wa Iran lilishambuliwa na magaidi lilipokuwa likipita katika barabara ya Khash-Zahedan katika mkoa wa Sistan na Baluchistan, kusini mashariki mwa Iran, ambapo askari 27 waliuawa shahidi na wengine 13 kujeruhiwa.
Kundi la kigaidi linalojiita "Jayshul Adl" lilidai kuhusika na hujuma hiyo. Kundi hilo lina mfungamano mkubwa na magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na kufadhiliwa na Saudi Arabia.