Rais Rouhani: Akthari ya mataifa ya dunia yanapinga vikwazo vya Marekani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hii leo ukiondoa nchi chache zenye fikra mgando katika eneo la Mashariki ya Kati pamoja na utawala haramu wa Israel, hakuna nchi nyingine inayounga mkono vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na hata waitifaki wa Magharibi wa Washington nao wanaamini kuwa, tangu awali uamuzi wa kutekeleza vikwazo hivyo haukuwa sahihi.
Rais Rouhani amesema hayo leo akiwa katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran na kubainisha kwamba, katika kipindi cha miaka Arubaini iliyopita daima Iran imekuwa ikiandamwa na vikwazo na kubainisha kwamba, Ulaya, Asia, Afrika, Amerika ya Latini na hata Amerika ya Kaskazini na ndani ya utawala wa Marekani kuna upinzani dhidi ya hatua za serikali ya Trump dhidi ya Iran.
Rais Hassan Rouhani ameeleza kuwa, wananchi wa Marekani nao wanaamini kwamba, Rais Donald Trump wa nchi hiyo hana haki ya kuiwekea vikwazo Iran na ufahamu na uelewa wa fikra za waliowengi ulimwenguni kuhusiana na haki ya Iran ni neema kubwa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria mafanikio ya taifa hili katika Mashariki ya Kati na kusema kuwa, katika historia ya eneo na ulimwenguni kwa mara ya kwanza kumechukuliwa uamuzi athirifu kwa ajili ya usalama wa eneo hususan kuhusiana na Syria, uamuzi ambao ulichukuliwa na nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki.
Rais Rouhani ameashiria pia mikutano ya pande tatu ya Iran, Russia na Uturuki yenye lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria na kuongeza kwamba, Iran ni moja ya mihimili mikuu ya kulinda na kuhifadhi usalama wa eneo hususan Syria.
Kadhalika Rais Rouhani amebainisha kuwa, Iran haiwezi kupuuza masuala yanayozihusu nchi jirani na kubainisha kwamba, kama kusingekuweko uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bila shaka Baghdad na eneo la Kurdistan ya Iraq yangekuwa yameangukia mikononi mwa kundi la kigaidi la Daesh.