Rouhani: Nchi za Magharibi hazikuhusika katika kungamizwa magaidi katika eneo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Watu wote wanajua kuwa, madola ya Magharibi hayajahusika hata kidogo katika jitihada za kuangamizwa magaidi katika eneo la Asia Magharibi na walirusha ndege na helikopta zao angani kimaonyesho tu.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo Jumanne katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad wakati alipohutubia kikao cha wasomi wa nchi hiyo. Rais wa Iran amebainisha lengo la madola makubwa ya kibeberu katika kuibua magaidi wakiwemo wa kundi la ISIS au Daesh katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) na kusema: "Kati ya malengo hayo ni kutaka kuzusha mgawanyiko na mifarakano baina ya nchi na mataifa ya eneo hilo, kuibua hitilafu kubwa baina ya makabila na madhehebu mbalimbali na kutetea uwepo wao haramu katika eneo hilo, kuzigawa vipande vipande Iraq, Syria na baadhi ya nchi na kujiarifisha kama mwokozi na hatimaye kuonyesha taswira isiyo sahihi kuhusu Uislamu."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza furaha yake kutokana na kuwa pamoja mataifa ya Iran na Iraq na mshikamano wao licha ya mazingira magumu katika eneo hili na kuongeza kuwa: "Katika vita dhidi ya magaidi wa ISIS, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa bega kwa bega na watu wa Iraq."
Rouhani amesisitiza kuwa, mataifa makubwa ya Iraq na Syria na watu walio macho katika eneo hili, wamezima njama zote za madola makubwa ya kiistikbari. Ameongoza kuwa: "Waislamu wa eneo la Asia Magharibi wameweza kuifahamisha dunia kuwa magaidi si Waislamu, na kinyume cha propaganda zinazofanywa na wenye chuki na Uislamu, Uislami ni dini ya uadilifu, rehema na kuishi pamoja kwa maelewano watu wa kaumu na dini zote.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kusema kuwa, mataifa yote ya Waislamu yana azma ya kuendeleza vita dhidi ya ugaidi hadi kuangamizwa fitina hiyo ya ugaidi Asia Magharibi. Rais Rouhani amesema, kuna haja ya kuwepo umoja na mshikamano kwa lengo la kujenga nguvu kubwa Asia Magharibi ili wakati madola ya kibeberu yanapoangazia eneo hili yasifikirie kupora utajiri wa mafuta.
Halikadhalika Rais wa Iran amesema uhusiano wa Iran na Iraq ni mzuri na wa kupigiwa mfano katika kanda hii na dunia nzima. Ametoa mfano kwa kusema, mamilioni ya Wairani na Wairaqi hutembeleana kila mwaka na nukta hiyo inaashiria ukuruba wa kihistoria na kiutamaduni baina ya mataifa haya mawili.