Mogherini: Hakuna kinachozuia ushirikiano wa kibenki kati ya Ulaya na Iran
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa maagizo mapya ya kiutekelezaji kwa ajili ya kushirikiana benki za Ulaya na Iran yameandaliwa na kwamba hakuna kizuizi chochote kinachozuia kutekelezwa ushirikiano wa nchi za Ulaya na Iran.
Akizungumzia kuhusu kuwepo benki za nje na ushirikiano wake na Iran kupitia Swift, Bi Federica Mogherini ameongeza kuwa baadhi ya benki hizo zimeonyesha hamu ya kutaka kushirikiana na Iran na kwamba siku chache zijazo benki nyingi muhimu za Ulaya zitaanza kushirikiana na Iran.
Mogherini pia amebainisha kuwa, kuwepo sekta za kibenki na kiuchumi za Ulaya nchini Ira ni kwa maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ulaya; na kwamba hakuna sababu yoyote itaipelekea Ulaya kuweka kizuizi katika uwanja huo.
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa katika ziara yake mjini Tehran, amekutana na kufanya mazungumzo muhimu na viongozi wa Iran kuhusu masuala ya pande mbili, kieneo na kimataifa na kwamba pande mbili zimekubaliana kushirikiana katika nyanja za elimu, nishati, usafirishaji, uchumi na suala la haki za binadamu. Mogherini pia ameutaja Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kuwa ni mafanio mzuri kwa ajili ya kutatua matatizo kimataifa na kuongeza kuwa, matamshi yanayotolewa na baadhi ya wagombea wa kiti cha urais nchini Marekani kuhusu kutengua mpango wa JCPOA ni propaganda tu. Amesema hii ni kwa sababu mpango wa JCPOA unatekelezwa na serikali ikiwemo ya Marekani yenyewe na kwa msingi huo hakuna watu wanaoweza kutengua mpango huo.