Rouhani: Quds ni mji mkuu wa kudumu wa Palestina na Golan haiwezi kutenganishwa na Syria
(last modified Sun, 07 Apr 2019 02:28:26 GMT )
Apr 07, 2019 02:28 UTC
  • Rouhani: Quds ni mji mkuu wa kudumu wa Palestina na Golan haiwezi kutenganishwa na Syria

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Quds ni mji mkuu wa kudumu wa Palestina na miinuko ya Golan ni ardhi ya Syria isiyotenganishika na ardhi nyingine za nchi hiyo na kwamba hatua yoyote iliyo kinyume na hivyo ni kukanyaga maamuzi wa Umoja wa Mataifa na ni kinyume na uhakika wa kihistoria.

Rais Rouhani alisema hayo jana (Jumamosi) katika kikao cha pamoja cha ujumbe wa ngazi za juu wa Iran na Iraq hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba Golan ni sehemu ya ardhi ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, hivyo hatua na mtazamo wowote ulio kinyume na hivyo, hauwezi kutia doa uhakika wake wa kihistoria.

Aidha ametilia mkazo wajibu wa kukomeshwa mauaji ya kizazi huko Yemen na kuongeza kuwa, hapana shaka hata chembe kwamba, utatuzi wa mgogoro wa Yemen ni wa kisiasa na ni matumaini yetu kuwa mazungumzo yataweza kurejesha amani na usalama nchini humo na kuruhusu misaada ya kibinadamu ya chakula na madawa kuwafikia wananchi wanaodhulumiwa wa Yemen.

Waziri Mkuu wa Iraq, Adil Abdul Mahdi al-Muntafiki akiwasiliana na watu mbalimbali pembeni mwa Rais Rouhani mjini Tehran

 

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Iraq, Adil Abdul Mahdi al-Muntafiki. Katika kikao hicho, Abdul Mahdi ameishukuru serikali na taifa la Iran kwa mapokezi mazuri iliyowapa wajumbe wa Iraq na kusisitiza kuwa, uhusiano wa Tehran na Baghdad utaimarishwa zaidi na zaidi, na hilo ndilo lengo la ziara yake hapa Tehran.

Vile vile amesema, uamuzi wa serikali mbili za Iran na Iraq wa kutoa visa bure baina ya raia wa nchi mbili ni uamuzi wa busara sana na kusisitiza kuwa, wananchi wa nchi hizo mbili ambao wana uhusiano wa karne nyingi, sasa wataweza kuimarisha zaidi ushirikiano wao katika nyuga zote kama za kibiashara, kiuchumi na kubadilishana wanafunzi.