Apr 18, 2019 12:49 UTC
  • Barua ya Zarif kwa walimwengu; uzushi wa Marekani ni hatari kubwa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezitaka serikali zote za dunia kuchukua msimamo wa kimsingi, imara na unaozingatia sherika katika kukabiliana na hatua ya Marekani ya kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH katika orodha yake ya makundi ya kigaidi.

Akiashiria matokeo hatari ya kisheria na kisiasa ya uzushi huo wa hivi karibuni wa Marekani wa kutaja sehemu ya jeshi rasmi la nchi inayojitawala na mwanachama wa Umoja wa Mataifa kuwa ya kigaidi, Muhammad Jawad Zarif amesema katika barua yake ya Jumatano kwa mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa nchi za dunia kwamba hatua hiyo ya Marekani ni moja ya matishio makubwa zaidi kwa mfumo wa dunia. Harakati za Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya mapatano ya kimataifa, upuuzaji wake wa sheria na taasisi za kimataifa, kuiondoa nchi yake katika mikataba na mashirika ya kimataifa na sasa kuweka sehemu ya jeshi rasmi la nchi inayojitawa katika orodha yake ya makundi ya kigaidi ni mambo yanayoonyesha wazi kwamba hatua za rais huyo si tu kwamba zinahatarisha usalama wa nchi moja bali ni hatari kwa usalama na amani ya dunia nzima. Mwenendo wa serikali ya hivi sasa ya Marekani unaonyesha wazi kwamba watawala wa nchi hiyo wanafuatilia siasa za upande mmoja zisizo na mpinzani wala mshindani.

Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Hatua hizo za upande mmoja za Trump ni hatari kubwa kwa usalama wa dunia ambapo kila nchi huru itakayochukua hatua za kupinga siasa za Marekani italengwa kwa njia moja au nyingine. Siasa za Trump tokea aingie White House hazitambui mipaka yoyote na amekuwa akizilenga taratibu nchi huru zinazopinga siasa zake, moja baada ya nyingine. Uingiliaji wa wazi wa Marekani katika nchi zinazojitawala kama vile Venezuela, maonyo ya nchi hiyo kwa Russia na Uturuki ili zibadilishe mienendo yao ni ishara ya wazi kwamba huenda katika siku zijazo nchi hiyo ikazichukulia hatua nchi nyingine zinazojitawala, kama ilivyofanya kuhusiana na Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika uwanja huo gazeti la Global Times la nchini China limeadika kuhusiana na hatua hiyo ya Marekani dhidi ya SEPAH kwamba, kwa kutumia vibaya neno 'uagaidi' Marekani inafanya njama za kuzidhoofisha nchi ambazo haizipendi. Kwa kutilia maanani hatua hizo hatari za Trump zinazohatarisha uthabiti na usalama wa dunia nzima, kuna udharura kwa ulimwengu kuchukua msimamo imara na wa pamoja kwa ajili ya kukabiliana na tabia hizo hatari za utawala wa Trump.

Mvutano wa Iran na Marekani

Ni wazi kuwa madhara ya upuuzaji wa Trump sheria za kimataifa hayatazikumba tu nchi fulani ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bali jamii nzima ya kimataifa. Miles Hanig, mwanaharakati wa masuala ya kisiasa wa Marekani anasema kwamba siasa za upande mmoja za Donald Trump ni tishio kwa Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa na kwamba zinachochea vita duniani. Akizungumzia suala hilo, Ghulamali Khushroo, mwakilishi wa zamani wa Iran katika Umoja wa Mataifa anasema kwamba siasa hizo za upande mmoja za Marekani zinakiuka sheria, misingi inayotawala katika Umoja wa Matifa na siasa za pande kadhaa na kusisitiza kwamba ulimwengu unapasa kusimama imara mbele ya siasa hizo hatari.

Tags