Rais wa Iran ampokea rasmi Waziri Mkuu wa Pakistan
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema leo asubuhi amempokea rasmi Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan katika Ikulu ya Saad Abad mjini Tehran.
Katika sherehe hizo za mapokezi rasmi, baada ya nyimbo za taifa za Iran na Pakistan, Waziri Mkuu wa Pakistan amekagua gwaride ya heshima.
Baada ya sherehe hizo, viongozi hao wawili wameanza mazungumzo rasmi. Kwa mujibu wa duru za kidiplomasia ajenda kuu ya mazungumzo baina ya Hassan Rouhani na Imran Khan imetajwa kuwa ushirikiano wa pande mbili katika nyuga za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan jana Jumapili aliwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran na kulakiwa rasmi na mkuu wa mkoa pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa mkoa wa Khurassan Razavi.
Alipowasili alifanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Khurassan Razavi Ali Reza Razm Hosseini kabla ya kufanya ziara katika Haram Takatifu ya Imam Ridha AS, Imam wa Nane wa Mashia mjini Mashhad.