Iran: Netanyahu anataka kuigeuza Bahrain kuwa kisiwa cha Israel
Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu anataka kuigeuza Bahrain kuwa kisiwa cha utawala huo wa Kizayuni.
Hossein Amir-Abdollahian ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina amesema hayo leo Jumanne katika ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, "Mbali na kutenda jinai dhidi ya wananchi wake, utawala wa Aal-Khalifa unataka kulisaliti taifa la Palestina.
Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa ameeleza bayana kuwa, Netanyahu anataka kuigeuza Bahrain kuwa kisiwa cha Israel, huku Riyadh ikitaka kuitwika Manama mzigo mzito wenye gharama kubwa wa kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa njama hizo za Marekani dhidi ya Waplestina kwa jina "Muamala wa Karne".
Mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani, Jared Kushner hivi karibuni alifichua kuwa, hatua ya kwanza ya 'Muamala wa Karne' itazinduliwa na Marekani nchini Bahrain katika 'Kongamano la Kiuchumi' la mwezi ujao wa Juni.
Mwezi uliopita, ujumbe wa kibiashara na kisiasa wa utawala wa Kizayuni wa Israel ulishiriki kwa siri kubwa Mkutano wa Kimataifa wa Kiuchumi wa Manama nchini Bahrain licha ya waandalizi wa mkutano huo kudai kuwa Wazayuni hao hawataushiriki kutokana na sababu za kiusalama.
Hossein Amir-Abdollahian amesema kimya cha jamii ya kimataifa na baadhi ya nchi za Kiislamu na Kiarabu ni moja ya sababu ambazo zimepelekea utawala wa Kizayuni uendelee kuwafanyia jinai za kutisha wananchi madhulumu wa Palestina na kusisitiza kuwa mpango huo uliopewa jina la Muamala wa Karne bila shaka utagonga mwamba.
Wapalestina wamekuwa wakiulaani na kuupinga vikali mpango huo wa 'Muamala wa Karne' wakiutaja kuwa ni moja ya njama kubwa zaidi dhidi ya taifa madhulumu la Palestina linalokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.