Rouhani: Taifa la Iran halitanyenyekea madola ya kibeberu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53635-rouhani_taifa_la_iran_halitanyenyekea_madola_ya_kibeberu
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ustawi na maendeleo ya taifa la Iran ni matokeo ya muungano wa kaumu zote na jamii za waliowachache nchini na kuongeza kuwa: "Taifa la Iran halitayanyenyekea madola ya kibeberu."
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
May 21, 2019 23:18 UTC
  • Rouhani: Taifa la Iran halitanyenyekea madola ya kibeberu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ustawi na maendeleo ya taifa la Iran ni matokeo ya muungano wa kaumu zote na jamii za waliowachache nchini na kuongeza kuwa: "Taifa la Iran halitayanyenyekea madola ya kibeberu."

Rais Hassan Rouhani aliyasema hayo Jumanne wakati wa kuzindua miradi ya maji katika mkoa wa Azerbaijan Magharibi katika eneo la magharibi mwa Iran na kuongeza kuwa: "Nguvu za taifa la Iran ni kubwa kiasi kwamba punde baada ya maadui kulitisha taifa hili wamelazimika kutangaza kuwa hawataki vita."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: "Taifa la Iran ambalo limeungana na lina imani thabiti daima limekuwa likisimama kidete mbele ya maadui na nukta hii inashuhudiwa siku zote miongoni mwa wananchi."

Rais Rouhani ameendelea kusema kuwa, njama za maadui zimewasababishia watu wa Iran matatizo na kuwaweka chini ya mashinikizo lakini akasisitiza kuwa mashinikizo hayo hayawezi kuwasambaratisha Wairani. Aidha amesema pamoja na kuwepo matatizo na mashinikizo hayo, taifa la Iran kamwe halitasalimu amri.

Akiwa safarini katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki, Rais Rouhani amezindua miradi 27 ya maendeleo na uwekezaji.

Katika siku za hivi karibuni Marekani imezidisha vitisho na mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku ikieneza propaganda za hujuma ya kijeshi dhidi ya nchi hii.

Msuguano baina ya Iran na Marekani ulianza mwezi Mei 2018 baada ya Rais Trump kuiondoa nchi yake katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Baada ya hapo Washington ilirejesha tena vikwazo dhidi ya Iran hatua ambayo inaendelea kulaaniwa kimataifa. Marekani sasa imeanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran kwa kutuma meli zake za kivita katika eneo.