Rouhani: Iran itaendelea na muqawama wake hadi Marekani irejee katika mkondo sahihi
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kufungamana na sera yake ya muqawama hadi pale Marekani itakaporejea katika mkondo ulio sahihi na ikiri kuwa ilikuwa imefuata mkondo mbaya.
Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumapili alipohutubia kundi la wanaakademia na madaktari hapa mjini Tehran ambapo alisisitiza kuwa, Iran inaweza kuketi kwenye meza ya mazungumzo kujaribu kupatia ufumbuzi suala lolote madhali adui atarejea katika njia iliyo sawa.
Amebainisha kuwa, upande ambao ulijiondoa kwenye meza ya mazungumzo na kwenye mapatano (ya nyuklia ya JCPOA) una wajibu wa kufuata njia iliyo sahihi na kujirudi.
Rais Rouhani ameeleza bayana kuwa, "Mimi kama mwakilishi wa taifa la Iran natangaza bayana kuwa, madhali adui hataonesha kujuta kutokana na uamuzi wake wa huko nyuma, sisi hatuna chaguo jingine ghairi ya kuendelea kuonyesha muqawama."
Dakta Rouhani ameashiria hali ya kukanganyikiwa na kutoa misimamo ya kukinzana Marekani na kusisitiza kuwa "Adui baadhi ya nyakati anaweka masharti ya kufanya mazungumzo na Iran, lakini hivi karibuni tumewaskia wakisema hawataweka masharti."
Matamshi ya Rais wa Iran yametolewa masaa machache baada ya Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kudai kuwa Marekani ipo tayari kufanya mazungumzo na Iran pasi na masharti, huku akionekana kulegeza kamba katika nukta 12 alizozitangaza huko nyuma, kama masharti ya kurejea katika meza ya mazungumzo na Tehran.
Pompeo aliyasema hayo jana Jumapili katika kikao na waandishi wa habari nchini Uswisi na kueleza kuwa, "Tuko tayari kufanya mazungumzo bila masharti yoyote, tuko tayari kuketi chini nao (Iran)."