Iran yaonya kuhusu matokeo mabaya ya ugaidi wa kiuchumi wa Marekani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amevitaja vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya taifa hili kama 'ugaidi wa kiuchumi', huku akitahadharisha kuhusu taathira hasi iwapo Washington itaendelea kung'ang'ania mkondo wake huo wa kuwashinikiza Wairani.
Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana Jumapili katika mahojiano na shirika la habari la ABC News na kubainisha kuwa, 'mashinikizo ya kiwango cha juu ya Marekani' yanawalenga moja kwa moja wananchi wa Iran na kwamba Tehran itatoa jibu mwafaka katika kujilinda.
Bila kutoa maelezo ya kina kuhusu taathira zenyewe, Dakta Zarif ameeleza bayana kuwa, "Iwapo Marekani itawasababishia Wairani maumivu makali kutokana na vita vyake vya kiuchumi sambamba na kuielekezea Iran ugaidi wa kiuchumi, bila shaka kutakuwa na matokeo mabaya."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, "Sisi hatutofautishi kati ya vita vya kiuchumi na vita vya kijeshi."
Dakta Zarif ameongeza kuwa, utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani katu hautafanikiwa kufikia malengo ya sera zake batili kwa kulishinikiza taifa la Iran.
Amesema serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina jukumu na wajibu wa kuwalinda Wairani kutokana na mashinikizo dhidi yao.