Leo ni kumbukumbu ya siku ya kufariki dunia Imam Khomeini MA
Jumanne ya leo ya tarehe 14 Khordad 1398 Hijria Shamsia inayosadifiana na tarehe 4 Juni 2019 Milaadia na ambayo kwa mwaka huu imesadifiana na tarehe 29 Ramadhani 1440 Hijria Qamaria ni siku ya kukumbuka mwaka wa 31 wa kufariki dunia Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Miaka 30 iliyopita katika siku kama ya leo, Imam Ruhullah Musawi Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87.
Imam Khomeini MA alianzisha mapambano yake dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah nchini Iran tangu mwaka 1963. Utawala wa kifalme wa Shah uliokuwa unaungwa mkono na Marekani haukuweza kuvumilia ukosoaji wa mwanachuoni huyo mwanamapambano hivyo ulimuondoa kwa nguvu nchini Iran na kumpeleka Uturuki na baadaye nchini Iraq.
Mwanachuoni huyo mkubwa wa zaman hizi alipitisha miaka 13 nchini Iraq akiwa ubaidishoni. Alikitumia kipindi hicho kusomesha na kulea wanafunzi madhubuti huku akiendelea kuukosoa vikali utawala wa kidikteta na fasidi wa Shah wa nchini Iran.

Baada ya kushadidi ukosoaji na harakati za Imam Khomeini, viongozi wa Iraq walimlazimisha aondoke nchini humo na kuelekea Ufaransa, lakini aliendeleza mapambano yake hadi yalipofikia ushindi Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 nchini Iran.
Tangu yalipofikia ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, taifa hili la Kiislamu limekumbwa na mashinikizo na njama za kila namna za madola ya kibeberu hususan Marekani vikiwemo vita vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam Hussein na kuilazimisha Iran kupigana vita vya miaka minane katika mazingira magumu sana ya kususiwa ya kambi zote za mashariki na magharibi duniani.
Kumbukumbu za kifo cha mwanachuoni huyo mkubwa wa zama hizi hufanyika kila mwaka katika Haram yake toharifu iliyoko kusini mwa mji wa Tehran.