Iran yaliasa jeshi la Sudan likabidhi madaraka kwa raia
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kueleza kusikitishwa kwake na machafuko ya kisiasa nchini Sudan, imetoa mwito kwa Baraza la Mpito la Kijeshi kukabidhi madaraka kwa raia kama wanayoshinikiza wananachi wanaoandamana kwa miezi kadhaa sasa.
Msemaji wa wizara hiyo, Abbas Mousavi amesema hayo leo Jumanne na kuonya kuwa, iwapo hali itazidi kuwa mbaya, basi nchi hiyo inajiweka katika hatari ya kugeuzwa uwanja wa makabiliano na madola ya kibeberu.
Ameziasa pande zote husika za kisiasa nchini humo kutumia njia za kidemokrasia, mazungumzo ya kisiasa na diplomasia kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.
Kadhalika msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezionya nchi ajinabi dhidi ya kuingilia masuala ya ndani ya Sudan, akisisitiza kuwa kitendo chao hicho sio tu kitafanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi, lakini pia kitayapa fursa makundi ya kigaidi na yenye misimamo mikali kujipenyeza na kuendeleza harakati zao nchini humo.
Kadhalika Mousavi amebainisha kuwa: "Tunatumai kwamba, pande zote husika zitatumia mazingira ya sasa ya kuelekea katika sikukuu ya Idul Fitr kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini, kwa lengo la kurejesha hali ya utulivu, usalama na amani sanjari na kuhitimisha taharuki iliyopo."
Duru za habari zinasema watu wasiopungua 35 wameuawa katika wimbi jipya la utumiaji wa nguvu kupita kisiasa wa maafisa usalama wa Sudan dhidi ya waandamanaji wanaotaka kukabidhiwa madaraka kwa raia.