Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; 'Muqawama (ukakamavu)', siri ya ushindi dhidi ya adui
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaambia viongozi na wananchi wa Iran kutohadaika na ujanja wa kisiasa wa rais wa Marekani.
Akizungumza Jumanne alasiri mbele ya umati mkubwa wa wananchi katika Haram ya Imam Khomeini (MA) kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa 30 wa kuaga dunia mwanzilishi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu huku akibainisha kwamba adui ana mbinu na hila nyingi, zikiwemo za vitisho na za kutia tamaa, kwa ajili ya kufikia malengo yake, amesema, Wamarekani hawapasi kupewa fursa ya kukaribia, kujongea kwao si kuzuri na kila sehemu wanakokwenda, huwa wanaibua vita, ndugu kuuana, fitina, unyanyasaji, ukoloni na kudhalilisha watu.
Huku akiashiria taathira kubwa ya fikra ya kusimama imara na kupambana na adui, Kiongozi Muadhamu amesema; ni wazi kuwa mapambano yana gharama lakini gharama ya kusalimu amri mbele ya adui ni kubwa zaidi. Mapambano na kuwa macho mbele ya hila za adui, kumeliwezesha taifa la Iran kuvuka salama vizuizi na njama za maadui katika miaka 40 iliyopita, na hivyo kupata nguvu na mafanikio makubwa inapoingia katika muongo wake wa 50.
Mapambano na ukakamavu huo wa taifa la Iran ambao unatokana na fikra ya Imam Khomeini (MA), hii leo umeiwezesha Iran kufikia hatua ya kuwa na nguvu kubwa ambayo inamzuia adui kuishambulia. Jambo hilo limethibiti wazi katika siku za hivi karibuni ambapo licha ya Marekani kutoa mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi na kutishia kuishambulia kijeshi Iran lakini nguvu hizo za Iran zimeiogopesha na kuifanya irejee nyuma na kulegeza msimamo.
Ukakamavu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima umekuwa ikivunja njama za maadui na kuna mifano chungu nzima ya kuthibitisha ukweli huo katika historia ya miaka 40 ya umri wa Mapinduzi ya Kiislamu. Chuki ya maadui ambayo ilianza tokea mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu inatokana na muqawama wa kimantiki na kidini wa watu wa Iran. Fikra hiyo ya muqawama ambayo inapigania uhuru wa kujitawala, licha ya kuwa ina gharama zake lakini ni njia bora na ya kimantiki zaidi kwa kila taifa linalotaka kuwa na utambulisho wa kujitegemea na nguvu ya kuogopewa na adui.
Hilo ndilo jambo ambalo limelipelekea taifa la Iran kushinda kila kikwazo na hila zinazotumiwa na adui dhidi ya taifa hili. Ni ukakamavu huo wa taifa la Iran ndio umevunja mashinikizo yote ya kisiasa, kijeshi na kiuchumi ya Marekani na kuwafanya watawala wa nchi hiyo ya kibeberu walegeze misimamo yao ya kiuhasama dhidi ya taifa hili.
Timu ya kisiasa na kijeshi ya serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani ambaye alianzisha vikwazo vikali dhidi ya Iran mara tu baada ya kuiondoa nchi hiyo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, leo imelazimika kulainisha maneneo yake inapozungumzia suala la Iran, jambo ambalo linathibitisha wazi taathira ya chaguo la muqawama.
Kupitia muqawama huo, taifa la Iran limefikia maendeleo makubwa ya kielimu, kisiasa, kiuchumu na kijeshi na bila shaka kuendelea kwa uadui wa Marekani dhidi ya taifa hili kunatokana na maendeleo hayo katika kivuli cha kujitawala wananchi wa Iran. Kwa maneno ya Kiongozi Muadhamu: Fikra ya muqawama ndiyo silaha yenye nguvu zaidi ya taifa lolote lile.'