Rais Rouhani: Kamwe Iran haitotumbukia katika mkwamo kwa sababu ya mashinikizo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuashiria kwamba hatua ya Marekani ya kujiondoa katika matapatano ya nyuklia ya JCPOA haikuwa na matokeo mengine ghairi ya taathira hasi kwenye mahusiano na usalama wa nchi za eneo, amesisitiza kwamba kamwe nchi hii haitotumbukia kwenye mkwamo kupitia mashhinikizo.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo alipokutana na Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani ambaye yuko safarini mjini Tehran, ambapo amesisitiza kwamba usalama wa eneo kamwe hautapatikana kupitia mashinikizo na vikwazo dhidi ya taifa la Iran amesema kuwa, hatua ya Marekani ya kuiwekea nchi hii vikwazo vya kidhalimu, inapita katika njia ya ugaidi wa kiuchumi. Amebainisha kwamba kwa ajili hiyo ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikaamua kusimama imara mbele ya wale wanaozuia madawa na vyakula kwa ajili ya raia wa Iran. Akiashiria ahadi mbalimbali za viongozi wa nchi tatu za Ulaya yaani Uingereza, Ujerumani na Ufaransa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hasa kutokana na kushindwa kwao kufungamana na ahadi zao na pia kutofanya juhudi kwa ajili ya hatua za kufidia hasara iliyotokana na kitendo cha kujiodoa Marekani kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA amefafanua kuwa, iwapo nchi za Ulaya zinaamini kwamba mapatano hayo ni kwa maslahi ya mahusiano ya Iran na Umoja wa Ulaya na kustawisha amani, uthabiti na usalama wa eneo, basi zinatakiwa kufanya haraka kwa ajili ya kulindwa mapatano tajwa na kwa hatua za kivitendo.
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa baadhi ya madai kwamba eti nchi hii ina mpango wa kuunda silaha za nyuklia na amesema kuwa jambo hilo halina ukweli wowote na kwamba ripoti 15 za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) na zaidi ya hayo pia, fatwa ya Kiongozi Muashamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya kuharamisha silaha hizo, yote hayo yanabainisha uongo wa madai hayo. Kwa upande wake Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, ameeleza hatua ya Marekani ya kujiondoa katika mapatano ya JCPOA kuwa isiyo sahihi na kuongeza kuwa, Berlin ina tofautiana sana na Washington kuhusiana na siasa zake dhidi ya Iran. Aidha amesema kuwa Ujerumani inafanya jitihada kwa kushirikiana na nchi nyingine za Ulaya hususan Ufaransa na Uingereza kuyalinda mapatano hayo ya nyuklia. Amesisitiza kwamba, mtu yeyote anayefahamu vyema historia ya Iran atabaini kuwa stratijia za mashinikizo zaidi dhidi ya taifa la Iran haziwezi kuwa na matokeo chanya.