'Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vinalenga kuvuruga usalama wa eneo'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54067-'vikwazo_vya_marekani_dhidi_ya_iran_vinalenga_kuvuruga_usalama_wa_eneo'
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vinalenga kuvuruga usalama wa eneo zima la Asia Magharibi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2019 22:58 UTC
  • 'Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vinalenga kuvuruga usalama wa eneo'

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vinalenga kuvuruga usalama wa eneo zima la Asia Magharibi.

Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliyasema hayo Jumanne mjini Tehran alipokutana na Zainul Abidin Rashid, Mjumbe Maalumu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore. Ameongeza kuwa, Marekani imeingia katika vita vya kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na jambo hili ni chanzo cha kuongezeka taharuki katika eneo.

Araqchi ameendelea kusema kuwa, usalama wa eneo unajumuisha nukta kadhaa ambazo zote zinafungamana  na kuongeza kuwa, pasina kuwepo usitishwaji vita vya kiuchumi, utulivu na usalama hauwezi kutazamiwa kupatikana katika eneo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, kadhia pekee ambayo imeweza kutatuliwa kwa mazungumzo na udiplomasia ni kadhia ya nyuklia ya Iran lakini Marekani imetumia dalili zisizo za kimantiki kujiondoa katika mapatano hayo.

Kwa upande wake, Zainul Abidin Rashid, Mjumbe Maalumu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore aamesema mashinikizo ya vikwazo yanaziathiri nchi zote na ameongeza kuwa nchi yake inaunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA. Aidha ameelezea matumaini yake kuwa mashinikizo ya eneo yatapungua.

Ikumbukwe kuwa Mei 8 mwaka jana Trump alichukua uamuzi wa upande mmoja na kuondoa nchi yake katika mapatnao ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA. Baada ya hapo utawala wa Marekani ulitangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran na sasa baada ya hatua iliyo kinyume cha sheria ya kujiondoa katika JCPOA, Marekani imeomba mazungumzo mapya na Iran. Hatua hiyo ya Marekan inaendelea kulaani kimataifa.