Udiplomasiia amilifu wa Iran na Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54237-udiplomasiia_amilifu_wa_iran_na_uturuki
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu leo Alkhamisi amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake wa Iran, muhammad javad Zarif katika mji wa Isfahan ambako pande hizo mbili zimejadili masuala ya pande mbili na kikanda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2019 03:58 UTC
  • Udiplomasiia amilifu wa Iran na Uturuki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu leo Alkhamisi amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake wa Iran, muhammad javad Zarif katika mji wa Isfahan ambako pande hizo mbili zimejadili masuala ya pande mbili na kikanda.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Abbas Mousavi amesema kuwa, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu na Utuuruki wanashauriana kuhusu ushirikiano wa kiuchumi, mapatano ya pande mbili katika medani hiyo na hali ya sasa katika eneo la magharibi mwa Asia.

Iran na Uturuki ambazo ni nchi jirani na zenye taathira kubwa katika eneo la magharibi mwa Asia, zinalipa umuhimu mkubwa suala la kustawisha uhusiano wa kiuchumi na kufuatilia masuala ya kikanda. Masuala ya ushirikiano wa kiuchumi baina ya pande hizo mbili pia daima yamekuwa yakipewa umuhimu mkubwa, na marais wa nchi hizo mbili wamekuwa wakibadilishana mawazo kuhusiana na kadhia hii mara kwa mara. Mashauriano ya hivi karibuni kabisa baina ya marais wa nchi hizo mbili yalifanyika katika mkutano wa viongozi wa nchi za Asia uliofanyika Dushanbe huko Tajikistan tarehe 15 mwezi huu wa Juni. Katika mazungumzo hayo, Rais Hassan Rouhani wa Iran alimwambia mwenzake wa Uturuki kwamba, Tehran ina hamu kubwa ya kustawisha zaidi uhusiano na Ankara katika nyanja zote hususan katika masuala ya uchumi na biashara. Rais Rouhani alisema: Kuna udharura wa kufanyika jitihada za kuimarisha ushirikiano uliopo na kufikisha biashara ya kila mwaka kati ya nchi hizi mbili kwenye kiwango kilichoafikiwa.

Rais Rouhani na mwenzake wa Uturuki Tayyip Erdoğan

Ilitazamiwa kuwa thamani ya biashara baina ya Iran na Uturuki itafikia dola bilioni 12 mwaka huu wa 2019. Lengo lililoainishwa na viongozi wa Iran na Uturuki ni kustawisha biashara ya pande hizo mbili hadi kufikia dola bilioni 30 kwa mwaka. 

Masuala yanayoyakutanisha pamoja mataifa ya Iran na Uturuki kama vile utamaduni, lugha na dini moja yanatayarisha njia na mazingira mazuri ya kustawisha zaidi uhusiano wa kiuchumi wa nchi mbili, na mikoa ya mpakani ina mchango mkubwa katika uwanja huo. Nchi zote mbili za Iran na Uturuki zimeonesha hamu na azma kubwa ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili na katika miaka ya hivi karibuni hususan baada ya kutiwa saini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kumechukuliwa hatua za maana katika uwanja huu. 

Katika mkondo huo huo Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alisema katika mazungumzo yake na Rais Rouhani katika mkutano wa Dushanbe kwamba: Uhusiano wa Iran na Uturuki ni mzuri katika nyanja zote na unaendelea kustawi, na suala la kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili linapewa umuhimu mkubwa na serikali ya Ankara.

Irada na azma kubwa ya kuimarisha uhusiano baina ya Tehran na Ankra hususan katika masuala ya uchumi na mtazamo unaofanana wa pande hizo mbili kuhusiana na matukio mengi ya kikanda na kimataifa ni ishara kwamba, Iran na Uturuki ni washirika wawili wa kistratijia wa kuaminika.

Mazungumzo ya marais wa Iran na Uturuki

Tehran na Ankara pia zimekuwa zikisisitiza udharura wa kulindwa usalama na amani ya eneo muhimu la magharibi mwa Asia na kupinga vikali siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani katika uga wa masuala ya kimataifa na vilevile kupinga vikwazo vya serikali ya Washington dhidi ya nchi mbalimbali.

Safari ya leo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki nchini Iran na mazungumzo ya Mevlüt Çavuşoğlu na mwenyeji wake, Muhammad Javad Zarif mjini Isfahan baada ya mazungumzo ya viongozi wa nchi hizo mbili huko Dushanbe ni kielelezo cha umuhimu wa mashauriano ya Iran na Uturuki katika mazingira na kipindi hiki.