Zarif: Iran italinda mipaka yake ya maji, ardhi na anga
Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Iran itatumia nguvu zake zote kulinda mipaka yake ya maji, ardhi na anga.
Zarif ameyasema hayo katika radiamali yake kufuatia kutunguliwa na kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ndege ya ujasusi ya Marekani isiyo na rubani baada ya ndege hiyo kukiuka anga ya Iran. Akielezea suala hilo kupitia ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, amesema: "Marekani ambayo imeiwekea Iran vikwazo vya kigaidi vya kiuchumi na kuendesha hatua za siri, sasa imekiuka anga ya Jamhuri ya Kiislamu." Amezidi kufafanua kwamba Iran imewasilisha ushahidi wa ukiukaji mpya wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa na utathibitisha kuwa Washington inasema uongo kuhusiana na sehemu ilikotunguliwa ndege hiyo.
Inafaa kuashiria kuwa, asubuhi ya jana Ofisi ya Mahusiano ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ilitangaza habari ya kusambaratisha ndege ya ujasusi ya Kimarekani, baada ya ndege hiyo kukiuka anga na ardhi ya Iran katika eneo la Kouh-e-Mobarak katika mkoa wa Hormozgan, kusini mwa nchi hii. Komandi ya kigaidi ya askari wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi (CENTCOM) sambamba na kukiri habari hiyo imedai kwamba ndege hiyo isiyo na rubani ya Marekani ilikuwa bado haijaingia katika anga ya Iran na kwamba eti ilikuwa katika maji ya kimataifa.