Iran: Tulitoa onyo mara chungu nzima kabla hatujaitungua ndege ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54261-iran_tulitoa_onyo_mara_chungu_nzima_kabla_hatujaitungua_ndege_ya_marekani
Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Khatamul Ambiyaa SAW cha Iran amesema kuwa, kutojali Wamarekani sheria za kimataifa ndiko kulikopelekea ndege yao ya kijasusi itunguliwe na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) hasa baada ya kudharau tahadhari na maonyo mengi yaliyotolewa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 21, 2019 06:09 UTC
  • Iran: Tulitoa onyo mara chungu nzima kabla hatujaitungua ndege ya Marekani

Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Khatamul Ambiyaa SAW cha Iran amesema kuwa, kutojali Wamarekani sheria za kimataifa ndiko kulikopelekea ndege yao ya kijasusi itunguliwe na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) hasa baada ya kudharau tahadhari na maonyo mengi yaliyotolewa.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Meja Jenerali Qader Rahimzadeh  akisema hayo leo na kuongeza kuwa, droni ya kijasusi ya Marekani imetunguliwa baada ya kudharau sheria za kimataifa na baada ya kutoka katika njia zilizoainishwa za kimataifa na kuingia katika maji ya Iran. Kulitolewa maonyo mara kadhaa kuitaka ndege hiyo itoke kwenye maji ya Iran lakini ilidharau n akwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imerekodi kila kitu kabla ya kuitungua kwa kombora ndege hiyo yakisasa kabisa isiyo na rubani ya Marekani.

Mabaki ya ndege ya kijasusi ya Marekani iliyotunguliwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH baada ya kuingia bila ya ruhusa katika anga ya kusini mwa Iran

Amesema, tabia ya kibeberu ya Washington na kutoheshimu kwake haki za wengine ndiko kulikopelekea kutunguliwa ndege hiyo ya kijasusi ya Marekani.

Alkhamisi alfajiri, ndege moja ya kijasusi isiyo na rubani ya Marekani aina ya Global Hawk ilitunguliwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH katika mkoa wa Hormozgan wa kusini mwa Iran baaada ya kuingia kinyume cha sheria katika anga ya Iran.

Baada ya kutunguliwa ndege hiyo ya kisasa kabisa na yenye thamani kubwa, viongozi wa Marekani wamekuwa wakieneza propaganda kwamba eti ndege hiyo ilitunguliwa ikiwa katika anga ya kimataifa, madai ambayo yanaendelea kukanushwa vikali na viongozi wa Iran ambao wanasisitiza kuwa wana ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha wanachokisema.

Ndege ya kijasusi ya Marekani ya Global Hawk