Zarif: Iran kamwe haitasahau uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Saddam
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54442-zarif_iran_kamwe_haitasahau_uungaji_mkono_wa_nchi_za_magharibi_kwa_saddam
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitasahau uungaji mkono wa nchi za Magharibi na misaada ya silaha za nchi hizo zikiwemo silaha za kemikali kwa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 29, 2019 12:10 UTC
  • Zarif: Iran kamwe haitasahau uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Saddam

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitasahau uungaji mkono wa nchi za Magharibi na misaada ya silaha za nchi hizo zikiwemo silaha za kemikali kwa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein.

Muhammad Javad Zarif leo Jumamosi ameweka katika ukurasa wake wa Twitter picha ya wahanga wa shambulio la kemikali lililofanywa na Saddam Hussein katika mji wa Sardasht kaskazini magharibi mwa Iran na kuandika: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikulaani shambulio hilo dhidi ya wananchi wa Iran. Zarif ameongeza kuwa wananchi wa Iran wakati huo pia walisimama kidete mbele ya maadui na hivi sasa pia watasimama imara dhidi yao.

Watu 119 waliuawa shahidi na wengine zaidi ya elfu nane kudhuruka kwa silaha za kemikali katika shambulio liliofanywa Juni 28 mwaka 1987 na utawala wa zamani wa Iraq katika mji wa Sardasht mkoani Azerbaijan Magharibi nchini Iran. 

Wahanga wa shambulio la kemikali la Saddam Hussein katika mji wa Sardasht, Iran

Utawala mtenda jinai wa Saddam Hussein ulitumia silaha za kemikali mara kadhaa katika miaka yote ya kujiri vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Nyaraka na ushahidi uliotolewa katika miaka ya mwisho ya kumalizika vita hivyo ulionyesha kuwa makampuni 207 ya nchi za nchi za Magharibi zikiwemo Marekani, Uholanzi, Ujerumani na Ufaransa yalikuwa yakiupatia silaha za kemikali utawala wa Baath wa Iraq.