Waislamu waomboleza mauaji ya mjukuu wa Mtume, Sadiq Aali Muhammad
(last modified Sat, 29 Jun 2019 16:55:59 GMT )
Jun 29, 2019 16:55 UTC
  • Waislamu waomboleza mauaji ya mjukuu wa Mtume, Sadiq Aali Muhammad

Waislamu wa Iran na baadhi ya maeneo mengine ya dunia leo tarehe 25 Mfunguo Mosi Shawwal wameshiriki katika shughuli ya kukumbuka na kuomboleza mauaji ya mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ja'far Sadiq (as).

Hapa nchini Iran shughuli hiyo ya maombolezo imefanyika katika misikiti, maeneo ya kidini na kumbi za shughuli za kijamii kwa majlisi na vikao vilivyohutubiwa na maulamaa na mahatibu waliowakumbusha Waislamu juhudi kubwa zilizofanywa na Imam Ja'far Swadiq (as) kuhuisha mafundiyo ya babu yake.

Shughuli za maombolezo hayo zilikuwa kubwa zaidi katika miji miwili mitakatifu ya Qum na Mash'had ambako maelfu ya Waislamu waliokuwa wamevaa mavazi ya rangi nyeusi walionekana katika hali ya huzuni na majonzi wakikumbushana maafa yaliyompata Imam wa Sita katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw). 

Waislamu katika majlisi ya kukumbuka mauaji ya Imam Sadiq (as), Mash'had

Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiumawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu. Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabir bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (as). 

Mjukuu huyo wa Mtume Mtukufu amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake, aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi Mansur al Dawaniqi mwaka 148 hijria na kuzikwa katika mji mtakatifu wa Madina. 

Tags