Jul 12, 2019 14:03 UTC
  • Muhammad Javad Zarif
    Muhammad Javad Zarif

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kusimamishwa meli ya mafuta ya Iran katika lango bahari la Jabal Tariq (Gibraltar) ni kielelezo cha utegemezi wa Uingereza kwa Marekani.

Muhammad Javad Zarif ameambia televisheni ya al Mayadeen ya Lebanon kwamba: Hatua ya Uingereza ya kusimamisha na kushikilia meli ya mafuta ya Iran ni uharamia, na kwa hatua hiyo Uingereza imetangaza rasmi kwamba ni kibaraka wa Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: Wamarekani wamemdhalilisha Waziri Mkuu wa Uingereza kwa sababu tu ya London kutangaza kwamba, inamuunga mkono balozi wake mjini Washington (baada ya kuvujishwa maandishi yake yaliyomkosoa Donald Trump).

Jeshi la majini la Uingereza tarehe 5 mwezi huu wa Julai lilisimamisha na kushikilia meli ya mafuta ya Iran kwa kisingizio kwamba, imekiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria. Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekadhibisha madai hayo ya Uingereza na kuitaka London iiachie mara moja meli hiyo ili iendelee na safari yake.

Meli ya mafuta ya Iran, Grace-1

Serikali ya Uingereza imeishikia meli hiyo ya mafuta ya Iran licha ya kwamba, haijakiuka sheria yoyote ya usafirishaji wa baharini na hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu za kisiasa na kwa kuchochewa na Marekani. Serikali ya Marekani, kwa kutumia sera zake za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, imeitaka Uingereza isimamishe meli hiyo ya mafuta ya Iran katika maji ya lango bahari la Jabal Tariq.

Punde baada ya kukamatwa meli hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Josep Borrell amesema kuwa: Jeshi la majini la Uingereza limesimamisha meli ya mafuta ya Iran katika maji ya eneo la lango bahari la Jabal Tariq kwa matakwa ya Marekani.

Meli hiyo ya Iran ingali inashikiliwa, na polisi ya eneo la Jabal Tariq ilidai Alkhamisi ya jana kwamba, nahodha na afisa mkuu wa meli hiyo wamekamatwa kwa tuhuma ya kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya.

Eneo la Jabal Tariq linalokaliwa kwa mabavu na Uingereza

Mchezo wa kisiasa wa serikali ya Uingereza unaonesha jinsi nchi hiyo ambayo imo mbioni kujitenga na Umoja wa Ulaya, inavyozidi kuwa tegemezi kwa Marekani. Suala hili linaonekana wazi zaidi kwa hatua hii ya London ya kutekeleza sera za vikwazo haramu za serikali ya Washington dhidi ya nchi nyingine ambazo zimekuwa zikipingwa na Umoja wa Ulaya.

Urafiki na ushirikiano wa Uingereza na Marekani hauishii katika kadhia hii ya kushikiliwa meli ya mafuta ya Iran, bali unaonekana katika kipindi chote cha historia ya kisiasa ya Uingereza dhidi ya Iran. Mfano mzuri wa ushirikiano huo ni suala la kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran katika kipindi cha serikali ya Dakta Musaddeq. Wakati huo serikali ya Uingereza ilizuia uuzaji wa mafuta wa serikali ya wakati huo ya Iran. Hivi sasa pia usimamishaji wa meli ya mafuta ya Iran katika lango bahari la Jabal Tariq kwa kisingizio cha kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria ni utekelezaji wa sera za vikwazo haramu na vya upande mmoja vya Marekani ambavyo lengo lake kuu ni kuzuia kabisa uuzaji wa mafuta ya Iran nje ya nchi.

Donald Trump

Kwa vyovyote vile hatua hiyo ya Uingereza inapingana na misimamo iliyotangazwa na serikali ya London eti ya kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Kwani kulindwa makubaliano hayo kunalazimu kudhaminiwa maslahi ya kiuchumi ya Iran na hapana shaka kuwa uuzaji nje wa bidhaa ya mafuta ni msingi mkuu wa maslahi hayo. Inasikitisha sana kuona kuwa, badala ya kuisaidia Iran kuuza mafuta yake nje ya nchi kwa mujibu wa vipengee vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Uingereza imeamua kujiunga na Marekani na kufanya ugaidi wa kiuchumi dhidi ya Iran.

Tags