Ali Shamkhani: Iran itaendelea kuunga mkono muqawama wa Palestina hadi utakapopata ushindi
(last modified Tue, 23 Jul 2019 12:30:38 GMT )
Jul 23, 2019 12:30 UTC
  • Ali Shamkhani: Iran itaendelea kuunga mkono muqawama wa Palestina hadi utakapopata ushindi

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuiunga mkono Palestina hadi muqawama utakapopata ushindi mbele ya utawala unaoua watoto wa Israel.

Ali Shamkhani amesema hayo leo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Saleh al-Arouri, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na kueleza bayana kwamba, uungaji mkono kwa malengo matukufu ya Palestina chimbuko lake ni misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, mpango unaojulikana kwa jina la 'Muamala wa Karne' ni hatua iliyoshindwa na kugonga mwamba na katu mpango huo hauwezi kutekelezeka.

Shamkhani aidha amesema kuwa, utawala haramu wa Israel na washirika wake, wamo katika hali ya kulegalega na kusambaratika na bila shaka mipango bandia ambayo inapingana na matakwa pamoja na irada ya wananchi wa Palestina katu haiwezi kufanikiwa.

Ali Shakhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (kulia) katika mazungumzo yake na Saleh al-Arouri, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS

Kadhalika Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu waliokuwa wakifanya njama za kuzusha hitilafu baina ya makundi ya muqawama na waungaji mkono wakuu wa Palestina hii leo wana ushirikiano na Israel na wamekuwa wakipata msaada wa washauri wa kijeshi wa Israel katika kuwaua wananchi Waislamu.

Kwa upande wake  Saleh al-Arouri, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amepongeza uungaji mkono wa Iran kwa muqawama wa Palestina na kusisitiza kuwa, taifa la Palestina haliogopi vitisho vya Israel.

Tags