Meja Hussein Salami: Hakuna ndege yoyote isiyo na rubani ya Iran iliyotunguliwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54974-meja_hussein_salami_hakuna_ndege_yoyote_isiyo_na_rubani_ya_iran_iliyotunguliwa
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) aliyekuwa ametembelea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko ya mkoa wa Lorestan, amesema: "Natangaza rasmi kuwa hakuna ndege yoyote isiyo na rubani ya Iran iliyotunguliwa."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 24, 2019 23:18 UTC
  • Meja Hussein Salami: Hakuna ndege yoyote isiyo na rubani ya Iran iliyotunguliwa

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) aliyekuwa ametembelea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko ya mkoa wa Lorestan, amesema: "Natangaza rasmi kuwa hakuna ndege yoyote isiyo na rubani ya Iran iliyotunguliwa."

Meja Jenerali Hussein Salami ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari ambapo sambamba na kubainisha kwamba iwapo maadui wana ushahidi wowote kuhusiana na kadhia hiyo basi wathibitishe, amefafanua kuwa, ndege isiyo na rubani ya Iran ilipaa kwa muda wa saa 3 na dakika 40 katika anga ya maji ya Ghuba ya Uajemi na kutuma moja kwa moja picha za meli za kieneo na za kimataifa, ambapo baadhi ya picha hizo zimeonyeshwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) kwa wananchi wa Iran na kwa walimwengu wote. Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ameongeza kwamba katika dunia ya leo hakuna mtu anayeweza kukubali maneno yasiyo na ushahidi, iwapo maadui wanayo video ya kutunguliwa na vipande vya ndege hiyo inayodaiwa kuwa ya Iran, basi waionyeshe.

Trump, muongo aliyeshindwa kuthibitisha madai yake

Amezidi kusisitiza kuwa: "Huo ni uongo mkubwa na sisi tumeonyesha kuwa ni uongo, hivyo maadui nao wathibitishe madai yao." Hii ni katika hali ambayo Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Iran pia akizungumza na waandishi wa habari kando ya kikao cha baraza la mawaziri amejibu madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kwamba jeshi la nchi hiyo limetungua ndege isiyo na rubani ya Iran. Akibainisha suala hilo Amir Hatami amesema: "Ndege isiyo na rubani ya Iran ilitekeleza majukumu yake na kurejea kwa amani katika eneo lake, na kama kuna mtu anayedai kinyume na hivyo basi na athibitishe madai yake  kama tulivyofanya sisi baada ya kutungua ndege ya kijasusi ya adui."