Zarif akosoa siasa za kindumakuwili za serikali ya Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa siasa na mienendo ya kindumakuwili ya Marekani kuhusiana na Iran na nchi tegemezi kwa serikali ya Washington.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Muhammad Javad Zarif ameiashiria Saudi Arabia kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kusema: Iwapo utaua Wamarekani zaidi ya elfu tatu lakini unaendelea kuwa mteja wa Washington, unaweza kumiliki silaha za nyuklia.
Zarif ameongeza kusema kuwa: Kinyume chake, nchi zisizosalimu amri mbele ya matakwa ya timu "B" (inayoundwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia Muhammad bin Salman na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani John Bolton), haziruhusiwi hata kuwa na nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria pia nafasi na mchango mkubwa wa Iran katika kupambana na makundi ya kigaidi na kusema: Wakati Iran inapambana na magaidi wa kundi la Daesh, nchi tegemezi kwa Marekani zimekuwa zikilizatiti kundi hilo kwa silaha na zana za vita.