Vikwazo, gharama ya "hapana" ya Dakta Zarif kwa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55225-vikwazo_gharama_ya_hapana_ya_dakta_zarif_kwa_marekani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria safari yake ya mwezi uliopita huko mjini New York na kusema kuwa, "niliambiwa nitawekewa vikwazo katika kipindi cha wiki mbili zijazo isipokuwa kama nitakubali kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani."
(last modified 2026-08-14T10:24:44+00:00 )
Aug 06, 2019 20:47 UTC
  • Vikwazo, gharama ya

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria safari yake ya mwezi uliopita huko mjini New York na kusema kuwa, "niliambiwa nitawekewa vikwazo katika kipindi cha wiki mbili zijazo isipokuwa kama nitakubali kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani."

Dakta Muhammad Javad Zarif alisema hayo siku ya Jumatatu katika mkutano wake na waandishi wa habari na kueleza kwamba, licha ya Wamarekani kudai na kupigia debe uhuru wa kutoa maoni, lakini hawana imani na kitu hicho. Dakta Zarif ameongeza kuwa, hakuna wakati ambao mazungumzo na diplomasia yanafikia tamati na kwamba, ataendelea na harakati zake.

Tarehe Mosi mwezi huu wa Agosti, Wizara ya Fedha ya Marekani ilichukua hatua ambayo iko mbali na mantiki na hekima kwa kuliweka jina la dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika orodha ya Washington ya watu waliowekewa vikwazo. Tangu Rais Donald Trump aliposhika hatamu za uongozi nchini Marekani amekiuka mara chungu nzima sheria na kanuni za kimataifa sambamba na kuitoa nchi hiyo katika mikataba kadhaa ya kimataifa, ambapo makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni moja tu ya mikataba hiyo. Hatua hiyo ya Trump imewashangaza mno walimwengu.

Hatua ya Dakta Zarif ya kuweka bayana utambulisho na sababu ya yeye kuwekewa vikwazo na Marekani kimsingi amebainisha moja ya changamoto za serikali ya Washington. Kwa hakika matamshi ya Zarif yanaashiria nukta moja ambayo huenda ikawa si jambo jipya kwa fikra za waliowengi kutokana na jinsi wanavyomfahamu Trump. Hata hivyo bila shaka mwenendo na hatua hii ya Marekani imeisikitisha mno jamii ya kimataifa.

Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran

Serikali ya Marekani baada ya kujitoa katika mikataba na jumuiya za kimataifa na kuyatusi na kuyadhalilisha mataifa mengine na hata kuwaita watawala wa Kiarabu wa Mashariki ya Kati kuwa ni 'ng'ombe wa maziwa' sambamba na kumuita Rais wa Ufaransa Emannuel Macron kwamba ni 'mjinga' inataka kuwafikisha walimwengu ujumbe huu kwamba, Washington inaweza kuzitwishwa nchi nyingine ubeberu wake. Hata hivyo, Dakta Zarif akiwa kiongozi wa chombo cha udiplomasia cha Iran na kwa kuangalia uhalisia wa kisiasa, amewakumbusha na kuwatanabahisha walimwengu utambulisho halisi wa Marekani.

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Dakta Zarif alisisitiza kuwa, zama za mahubiri ya lugha za kibabe na utumiaji mabavu zimemalizika na kubainisha kwamba, Marekani haina ubavu wa kuanzisha muungano hata katika maeneo ambayo ina satwa na ushawishi, na nchi moja baada ya nyingine zimekuwa zikijitoa na kujiweka kando na Marekani kutokana na kuona aibu  ya kuhesabiwa kuwa ziko katika faharasa ya nchi zilizoko pamoja na Washington.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kusisitiza juu ya ulazima wa kupanuliwa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ameeleza kwamba, kuna udharura wa kuweko mazungumzo baina ya Iran na Iraq na nchi tatu wanachama wa baraza hilo, kuanzishwa Jukwaa la Mazungumzo ya Kieneo sambamba na kutiwa saini mkataba wa kutoshambuliana. Ameongeza kuwa, mazungumzo ni kwa manufaa ya Saudi Arabia, Imarati na nchi zote za eneo na akasisitiza ulazima wa kuanza mazungumzo hayo.

Katika mahojiano aliyofanyya hivi karibu na vyombo vya habari vya Marekani mjini New York, Dakta Muhammad Javad Zarif aliashiria shauku ya kutaka vita ya  'Timu B' inayoundwa na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani John Bolton, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia na Bin Zayed mrithi wa kiti cha ufalme wa Imarati (UAE)  na kusema kuwa, timu hiyo inataka kuiingiza Marekani katika vita na Iran.

 'Timu B' inayoundwa na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani John Bolton, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia na Bin Zayed mrithi wa kiti cha ufalme wa Imarati (UAE) 

Robert Edwards Hunter, balozi wa zamani wa Marekani katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO  anasema: Kumuwekea vikwazo mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa nchi hasimu au hata nchi adui ni jambo lisilokubalika kiakili na hatua hiyo inakiuka misingi na ada zote zilizoenea za kidiplomasia.

Washauri na wasaidizi wa Trump walitaraji kwamba, diplomasia ya Iran ingeogopa vitisho vya Marekkani, lakini hilo limekuwa ni ndoto za alinacha. Dakta Zarif ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kwamba: Ni fakhari kubwa kwangu, kuwekewa vikwazo kwa kosa la kulitetea taifa shujaa la Iran.